Wataalam wa Benki ya Dunia wakagua miradi ya Tanzania ya Kidijitali

DAR-Timu ya Benki ya Dunia ikiongozwa na Bw. Paul Seaden leo Julai 24, 2025 imekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania Project-DTP), ukiwemo mradi wa Kituo cha Ubunifu wa TEHAMA katika eneo la Biashara Mtandao (E-commerce Innovation Hub).
Vilevile, mradi wa Huduma Pamoja (One Stop Service Center) inayosimamiwa na Shirika la Posta Tanzania jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo imefanyika leo Julai 24, 2025 ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambao unalenga kuimarisha huduma za kidijitali nchini kwa kuwafikishia wananchi huduma muhimu kwa njia ya kisasa na kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejikita katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya TEHAMA.

“Kupitia Shirika la Posta na Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, tunajenga kituo hiki cha Huduma Pamoja ambacho kitahusisha taasisi mbalimbali kama BRELA, NHIF, NIDA na nyingine, ili mwananchi aweze kupata huduma hizo kwa wakati mmoja na mahali pamoja,” alisema Bw. Mbodo.
Aidha, Bw. Mbodo aliongeza kuwa Kituo cha Ubunifu wa Biashara Mtandao kitawezesha vijana kubuni na kuendeleza suluhisho za kisasa katika sekta ya biashara mtandao, hivyo kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, kiongozi wa Timu ya Wataalam wa Benki ya Dunia, Bw. Paul Seaden, alisema wameridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo na namna ambavyo serikali imejipanga kusogeza huduma karibu na wananchi:

“Tumeridhishwa na maendeleo ya vituo hivi vinavyojengwa nchi nzima. Ni matumaini yetu kuwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali watanufaika na huduma hizi na kuona thamani halisi ya uwekezaji huu,” alisema Bw. Seaden.
Naye Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), Bw. Bakari Mwamgungu, alieleza kuwa jumla ya vituo 32 vinajengwa katika mikoa yote ya Tanzania na vinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025, huku uzinduzi rasmi ukitarajiwa kufanyika Januari 2026.

Hapo awali, timu hiyo ya Benki ya Dunia pia ilitembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Ubunifu wa TEHAMA (Innovation Hub) kilichopo katika Ofisi za Tume ya TEHAMA, Upanga jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news