DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amesema BoT na Benki Kuu ya Rwanda (NBR) zitaendelea kushirikiana na kujengeana uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya fedha na uchumi kiujumla ili kuhakikisha nchi zote mbili zinazidi kuimarika katika maeneo hayo.
Gavana Tutuba ameyasema hayo alipofanya mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu ya Rwanda,Bi.Soraya Hakuziyaremye leo Julai, 24,2025 alipotembelea ofisi za BoT jijini Dr es Salaam.
Msingi wa mazungumzo hayo ulikuwa ni kujadili namna gani Benki Kuu hizo mbili zitashirikiana na kubadilishana uzoefu katika maeneo ya Kusimamia na Kudhibiti Mifumo ya Malipo pamoja na Kuhifadhi Akiba ya Nchi kupitia ununuzi wa dhahabu.
Akizungumza katika mkutano huo ambao aliuhudhuria kwa njia ya mtandao, Gavana Tutuba amesema, Tanzania ina mifumo imara ya malipo ikiwemo TIPS kwa miamala midogo na TISS kwa mikubwa, ambayo ni mifano ya kuigwa na nchi nyingine barani Afrika.
Ameongeza kuwa,Benki Kuu inawezesha malipo ya hundi au malipo madogo ya kielektroniki kupitia mfumo wa malipo wa Tanzania Automated Clearing House (TACH), malipo ya nje ya nchi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia mfumo wa malipo wa East Africa Payment System (EAPS).
Pia,inasimamia mfumo wa malipokwa nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika ujulikanao kama SADC RTGS.
Kuhusu ununuzi wa dhahabu Gavana ameueleza kuwa BoT ilianza rasmi ununuzi wa dhahabu nchini kuanzia Oktoba 2024 na kufikia Juni 30, 2025 tayari imekwisha nunua tani 6.5 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wakubwa.
Kwa upande wake, Bi. Hakuziyaremye, ameipongeza BoT kwa kutengeneza TIPS kwa kutumia utaalamu wa ndani ya taasisi kitu ambacho kinaonesha ni kwa kiasi gani Benki Kuu imepiga hatua katika eneo hilo.
Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huu utasaidia kuimarisha udhibiti na usimamizi thabiti wa mifumo ya malipo kwa nchi hizi mbili hususan kutokana na ongezeko la matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.
Kikao hiko pia, kilihudhuriwa na Naibu Gavana, Bi. Sauda Msemo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo, Bi. Lucy Shaidi, pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka BoT.






