DAR-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefungua Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO), katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar Es Salaam.
Mhe. Kombo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema mkutano huo unajadili na kutathmini hali ya usalama, mafanikio na maendeleo ya kisiasa na kijamii, utekelezaji wa maamuzi ya vikao vilivyopita, pamoja na mikakati ya kuimarisha taasisi na mifumo ya usalama wa kikanda.
"Tunapotathmini mafanikio yaliyopatikana, tuendelee kuongozwa na misingi ya mshikamano, ushirikiano wa pamoja, na tukubali kuwajibika kwa dhati kwa mujibu wa Mkataba wa SADC na Dira 2050. Nina imani kuwa kupitia majadiliano yetu, tutajizatiti upya na kuthibitisha nafasi ya SADC kama kinara wa amani, umoja, na mchakato wa kuunganisha bara la Afrika,”amefafanua Mhe. Kombo.
Amesema,dhamira ya SADC ni kuendelea kudumisha mshikamano, amani na utulivu kupitia usuluhishi wa migogoro, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, pamoja na kushirikisha makundi maalum kama wanawake na vijana katika juhudi za upatanishi.
Mhe. Kombo pia ameukaribisha Ujumbe wa Waangalizi wa SADC -SEOM kuja kushuhudia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na kutoa salamu za heri kwa Jamhuri za Malawi na Seychelles, ambazo zinatarajia kufanya Mkuu mwezi Septemba.
Aidha, ameeleza kuwa SADC imeanza kutekeleza mkakati wa kupambana na rushwa kwa kuanzisha Kielelezo cha Juhudi za Kupambana na Rushwa, ambacho tayari kimejaribiwa katika nchi mbili wanachama ambazo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Mauritius na kuonesha mafanikio makubwa.
Naye Katibu Mtendaji wa SADC,Mhe. Elias Magosi amezisihi nchi wanachama kutekeleza majukumu yao sambamba na utekelezaji wa sera na mipango muhimu inayolenga kuimarisha amani, utulivu, na utawala bora katika ukanda wa SADC.“Katika dira yetu ya kuleta mshikamano wa kanda na maendeleo endelevu, dhamira yetu kuu ni kuhakikisha amani na usalama vinadumu,” amesema Mhe. Magosi.










