ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Zanzibar itaendelea kuwa daraja muhimu la kuiunganisha Afrika na ulimwengu katika masuala ya ubunifu, tafiti na uimarishaji endelevu wa elimu ya juu kwa ajili ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Mkutano wa Elimu ya Juu na Teknolojia Afrika (QS AFRICA FORUM 2025) uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege tarehe 3 Julai 2025.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa jambo muhimu ni kuwa na ushirikiano na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu barani Afrika na duniani, ili kutoa fursa ya kuunganishwa kwa vyuo kwa ajili ya kufanya tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuimarisha elimu ya juu.
Akizungumzia suala la teknolojia ya Akili Unde (AI),Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa,Zanzibar haipaswi kubaki nyuma katika matumizi ya teknolojia hiyo, lakini ni lazima ihakikishe kuwa inapata manufaa na faida zake, sambamba na kuhakikisha udhibiti wa athari zake kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa za kielimu.









