BAWACHA wamvaa Humphrey Polepole

DAR-Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Sharifa Suleiman, amemshambulia vikali aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM Taifa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, akimtaka kutoa ukweli kuhusu tukio la kupigwa risasi kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, badala ya kujidai ni mtetezi wa haki.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Sharifa amesema anashangazwa na kauli za hivi karibuni za Polepole zinazokosoa chama tawala na kutetea viongozi wa CHADEMA, ikiwemo kesi inayomkabili Lissu kwa tuhuma za uhaini.

“Ninashangazwa na Humphrey Polepole ambaye mara zote amekuwa akisema ‘tuwakatae wahuni’, leo hii amekuwa akimpenda Tundu Lissu na kujifanya kumtetea. Kama kweli una nia njema na unakiri ulishiriki maamuzi mengi wakati wa Magufuli, basi toka hadharani utuambie nani aliyempiga risasi Lissu,” amesema Sharifa.

Sharifa ameongeza kuwa, Polepole hawezi kudai kuungana na Watanzania wanaopinga dhuluma wakati akiwa sehemu ya waliokuwa wakihujumu CHADEMA kipindi cha nyuma.

“Usitupake mafuta nyuma ya chupa. Tunajua ulishiriki maamuzi makubwa dhidi ya chama chetu. Watanzania wakusamehe? Sawa, lakini kwanza sema ukweli- nani aliyempiga risasi Tundu Lissu. Vinginevyo, tuwapuuze wahuni, tuwakatae wahuni, kwa sababu wahuni bado wako kazini,” amesisitiza.

Humphrey Polepole, ambaye hivi karibuni alijiuzulu nafasi ya Balozi wa Tanzania nchini Malawi na kuvuliwa hadhi ya ubalozi, amekuwa akitoa matamko makali dhidi ya CCM na Serikali, akisisitiza umuhimu wa haki, demokrasia na kutaka kesi ya uhaini dhidi ya Lissu iondolewe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news