Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa RC Makalla

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla kusimamia kikamilifu maendeleo ya Mkoa wa Arusha, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa Kandanda unaojengwa kwaajili ya kutumika kwenye michuano ya Afrika ya Afcon mwaka 2027.
Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Jumanne ya Agosti 26, 2025 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma wakati akimuapisha, CPA Makalla pamoja na viongozi wengine aliowateua hivi karibuni.

Pia, Rais Dkt.Samia amewaagiza Wakuu wote wa Mikoa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi ili kuzijua kero zao pamoja na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.

"Tumeona haja ya kukurudisha serikalini ili uendelee kutumia ujuzi wako na uzoefu wa kuhudumia wananchi katika ngazi ya mkoa, wewe sio mgeni umeshakuwa Mkuu wa Mkoa Mbeya, Katavi, Mwanza, jijini Dar es Salaam na sasa Jiji la Arusha, nina hakika utaliweza vizuri sana. Nakutakia kila la kheri,"amesema Rais Dkt.Samia.

Aidha,Rais Samia pia amekumbusha umuhimu wa Mkoa wa Arusha, akiutaja kama kitovu cha Utalii na Diplomasia nchini, akisema kwa uzoefu wa CPA Makalla ana uhakika kuwa atasimamia masuala hayo na mazingira ya Mkoa wa Arusha kwa ujumla kwa kushirikiana na Viongozi na watendaji wengine ndani ya Mkoa wa Arusha.

Rais Samia pia amemtaka kuhamasisha wananchi wa Mkoa wa Arusha kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi za ujio wa mashindano ya AFCON kama sehemu ya kukuza uchumi binafsi na wa Taifa kwa Ujumla.

Kwa mara ya kwanza Tanzania, Kenya na Uganda watakuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2027 ambapo nchi 24 zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news