TANGA-Katika kuendeleza juhudi za kutoa elimu kwa makundi maalumu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo kwa viziwi mkoani Tanga kuhusu alama za utambuzi wa noti halali sambamba na namna sahihi ya kutunza fedha.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefunguliwa leo, Ijumaa Agosti 15, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi-Utawala na Rasilimali Watu mkoani Tanga, Bw.Sebastian Masanja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Batlida Buriani.
Bw. Masanja amewahimiza washiriki hao kuwa mabalozi wazuri wa elimu hiyo muhimu, ambayo itasaidia kupambana na usambazaji wa noti bandia, pamoja na kuimarisha utunzaji bora wa fedha, hatua itakayopunguza gharama zinazolipwa na serikali kwa uchapishaji wa noti mpya mara kwa mara.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA), Bw.Kelvin Nyema ameishukuru BoT kwa kuendelea kuwafikishia elimu hiyo kundi hilo maalumu, akisisitiza kuwa itasaidia kupunguza kesi zinazohusu kukutwa na noti bandia.