ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi wanasiasa kutumia majukwaa ya kisiasa kutangaza sera za vyama vyao kwa wananchi badala ya kueneza siasa za chuki.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 15,2025 alipotoa salamu kwa waumini wa dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Ijumaa na dua maalum ya kuwaombea viongozi wakuu wa nchi, iliyofanyika katika Msikiti wa Shaafi, Mbuyu Mnene, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, ni vema wanasiasa kuhubiri amani na kueleza namna watakavyowatumikia wananchi baada ya kupata ridhaa ya kuwaongoza, badala ya kutangaza siasa za chuki, matusi na mifarakano ndani ya jamii.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza viongozi wa dini na waumini kuiombea nchi amani hasa katika kipindi hiki ambacho kimebakia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu. Amesema bila amani hakuna jambo lolote la maendeleo linaloweza kufanikishwa.

















