BoT yatoa taarifa muhimu kwa taasisi ndogo za fedha Daraja la Pili

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chama cha Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha (TAMFI) pamoja na Umoja wa Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha (TAMIU) imetangaza rasmi kuanza kwa utaratibu wa ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuboresha nidhamu ya kujisimamia na mwenendo wa soko katika sekta ya watoa huduma ndogo za fedha nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 7,2025 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw.Emannuel Mpawe Tutuba.

"Miongoni mwa juhudi endelevu za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha na kuboresha usimamizi kwa watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili, Benki Kuu imeamua kutumia utaratibu wa usimamizi binafsi kwa kushirikiana na vyama vya watoa huduma ndogo za fedha.

"Utaratibu huu umeundwa ili kukamilisha mfumo wa sasa wa usimamizi wa Benki Kuu kwa kutumia uwezo wa vyama hivyo katika kufikia wanachama wao."

Gavana Tutuba amefafanua kuwa, kupitia ushirikiano huu na kwa kuzingatia mamlaka ya kisheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Vyama vya Watoa Huduma Ndogo za Fedha (TAMFI na TAMIU) vimepewa rasmi jukumu la kuwa taasisi zinazotumia Mbinu Elekezi Kujidhibiti, zenye wajibu wa kukuza na kusimamia mwenendo bora wa soko,utatuzi wa migogoro, na utekelezaji wa mbinu bora miongoni mwa wanachama wao.

"Benki Kuu itaendelea kutoa leseni kwa taasisi za Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili, kusimamia utekelezaji wa jumla na kusaidia TAMFI na TAMIU katika kuzingatia makubaliano yao, ili kuhakikisha wanaotoa huduma hizo wanajisimamia kwa kuzingatia masharti ya leseni zao, hivyo kuhakikisha utekelezaji mzuri na uzingatiaji wa viwango vya kisheria na vya kikanuni."

Gavana Tutuba ameongeza kuwa,taasisi zote za Huduma Ndogo za Fedha za Daraja la Pili zinalazimika kujiunga na TAMFI au TAMIU ndani ya kipindi cha miezi sita tangu tarehe ya
taarifa hii na kuzingatia makubaliano ya kujisimamia kwa kupitia utaratibu huu.

"Utekelezaji wa utaratibu huu unaonesha dhamira ya pamoja ya kuboresha mazingira ya Watoa Huduma Ndogo za Fedha ili yaaminike, yawe wazi na rafiki kwa watumiaji wa huduma hizo.

"Hivyo, Benki Kuu inawahimiza wadau wote na umma kwa ujumla kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika mpango huu muhimu wa kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na kukuza mfumo imara wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha nchini,"amefafanua Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news