CRDB yapongezwa kwa kuunga mkono jitihada za Serikali huduma jumuishi za fedha

DAR-Benki ya CRDB imepongezwa kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupanua wigo wa huduma jumuishi za fedha, kupitia uzinduzi wa hati fungani ya Al-Barakah Sukuk inayozingatia misingi ya Shari’ah.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Gavana wa Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, katika hafla ya uzinduzi wa hati fungani hiyo iliyofanyika Agosti 9,2025 jijini Dar es Salaam. 

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

“Napenda kuipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa. Mchango huu unajumuisha uwezeshaji wa sekta binafsi kupata mikopo kwa riba na masharti nafuu, pamoja na ubunifu wa bidhaa na huduma mpya za fedha kama hati fungani ya Al-Barakah Sukuk,” alisema Bi. Msemo.
Ameeleza kuwa, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025, jumla ya benki tano nchini zinatoa huduma za fedha zinazofuata misingi ya Shari’ah.

“Idadi ya akaunti za amana kwa misingi hiyo imeongezeka kutoka 223,081 mwezi Juni 2020 hadi 809,105, sawa na ongezeko la asilimia 263. Aidha, thamani ya amana imepanda kutoka shilingi bilioni 440 hadi shilingi trilioni 1.4, ongezeko la asilimia 216,” alisema.

Bi. Msemo pia amebainisha kuwa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama na ustahimilivu wa sekta ya kibenki, ikiwemo kufanya marekebisho ya Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018. Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge tarehe 30 Juni 2024.
Aidha, ameeleza kuwa Benki Kuu imekamilisha maandalizi ya Kanuni za Uendeshaji wa Huduma za Kibenki Zisizotoza Riba (Non-Interest Banking Business Regulations), ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika katika miezi michache ijayo.

Amesisitiza kuwa, dhamira ya Benki Kuu ni kuendelea kusimamia kwa karibu sekta ya fedha na kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ili kuweka mazingira bora kwa utoaji wa hati fungani za Sukuk, hatua itakayochochea zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news