DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Julai 27, 2025 liliwakamata watuhumiwa wawili, Mathias Charles Joakim (Chingila) Miaka 24, Mkazi wa Salasala Kinondoni na Kassim Abdallah (Kipae) miaka 30 mkazi wa Tegeta kwa tuhuma za kuvunja nyumba usiku na kuiba pesa taslimu Shilingi za Tanzania milioni 105 mali ya Xue Huaxion ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Huaren ya Salasala Kinondoni, Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 10, 2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambaye amesema baada ya upelelezi na kuhojiwa kwa kina pesa taslimu Tsh. Milioni 82 na dolla za Marekani 267 zilizoibwa zilipatikana na kwamba hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.Katika hatua nyingine Agosti 8, 2025 maeneo ya Tabata Matumbi Jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wapokeaji wa mali za wizi hasusan pikipiki ambao ni Hamad Mohamed Kamea (Mpemba) miaka 49 mkazi wa Kigogo na Abul Ramadhan Ally miaka 20 mkazi wa Yombo.
Amesema,walikutwa na pikipiki mbili zenye usajili wa MC 537 EWT aina ya Boxer na MC 951 ESS aina ya TVS ambazo ziliibwa maeneo tofauti tofauti. Hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.
SACP Muliro ameeleza kuwa,katika kipindi cha mwezi Juni hadi Julai 2025 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilifuatilia watuhumiwa waliokamatwa na baadae wakafikishwa mahakamani.
Pia,amesema yapo mafanikio hasa kwenye makosa ya ukatili kwa wanawake na watoto ambapo baadhi ya watuhumiwa wamepatikana na hatia ambao ni Musa Bakari (36) dereva, mkazi wa Mbezi Makabe alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti kwenye Mahakama ya Wilaya Kinondoni.
Khalifani Ramadhani (25) mkazi wa Kiponza Chamazi kwenye Mahakama ya Wilaya ya Temeke alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha (kisu).
Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi lao ili kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi katika mitaa mbalimbali jijini ili kuziba mianya ya wahalifu kutenda makosa.