DAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amechangia Shilingi Milioni 50 katika Mfuko Maalum wa Kampeni za CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Dkt. Mwinyi ametoa mchango huo katika Harambee hiyo iliyozinduliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika tarehe 12 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, naye amechangia Shilingi Milioni 100 katika Harambee hiyo, huku viongozi mbalimbali wa Serikali, Taasisi, Kampuni, Mashirika, makada na wanachama wa CCM wakitoa michango yao kwa moyo wa uzalendo.
Katika Harambee hiyo, jumla ya Shilingi Bilioni 56 zimekusanywa, na ahadi za michango yenye thamani ya Shilingi Bilioni 30 zimetolewa na taasisi na watu binafsi walioshiriki hafla hiyo.

















