DODOMA-Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe ameipongeza Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa kuendelea kuelimisha umma kuhusu majukumu yake hususani jukumu la kukinga amana katika benki na taasisi za fedha nchini.
Pongezi hizo amezitoa Agosti 8,2025 katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Nanenane Nzuguni jijini Dodoma baada ya kutembelea banda la DIB.Aidha,Mheshimiwa Bashe alipoulizia kuhusu ufilisi wa FBME, maafisa wa DIB wamemweleza kuwa,hadi sasa waliokuwa na amana katika benki hiyo wamekwishalipwa asilimia 55 ya madai yao kutokana na mali zilizokusanywa za FBME na kwamba zoezi la ufilisi, kwa maana ya kupata mali zaidi linaendelea.
Katika banda la Bodi ya Bima ya Amana, Mheshimiwa Bashe amepokelewa na kukaribishwa na viongozi na wafanyakazi na kuelezwa majukumu ya taasisi hiyo.Alipokewa na Meneja Uendeshaji wa DIB, Bw. Nkanwa Magina, Meneja wa Huduma za Kisheria, Bw. David Njau na wafanyakazi wa DIB na kuelezwa majukumu ya taasisi hii, hasa yanayohusiana na kukinga amana za wateja wa benki ili endapo benki zikifa waweze kupata fedha zao, ufilisi wa benki baada ya kuteuliwa na Benki Kuu, pamoja na kusimamia mfuko wa bima ya amana.
Aidha, Bw. Magina alimweleza Mheshimiwa Wziri kwamba wakulima, wafugaji na wavuvi ni wadau wakubwa wa Bodi ya Bima ya Amana kwa sababu wanapozalisha wanapata pesa na wanaweka katika benki, hivyo ni vema waelimishwe kwamba fedha zao zinakingwa kupitia Bodi ya Bima ya Amana.
Meneja Uendeshaji wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Bw. Nkanwa Magina akimpatia zawadi Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe baada ya kutembelea banda la DIB tarehe 8 Agosti 2025. Kulia kwa Bw.Magina ni Meneja Huduma za Kisheria wa DIB, Bw. David Njau na Afisa Mwandamizi Bi.Joyce Shala.Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ni taasisi ambayo kwa muda mrefu imekuwa sehemu ya Benki Kuu ya Tanzania na kwamba ni hivi karibuni imeanza kujitegemea katika baadhi ya majukumu.
Aidha, utendaji wa DIB unahusiana sana na Benki Kuu ambayo ina jukumu la kusimamia na kukagua benki na taasisi za fedha. Hata utekelezaji wa jukumu jipya la DIB la kupunguza hasara kwa benki, utategemea usimamizi wa benki unaofanywa na Benki Kuu.
Afisa Mwandamizi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Bi.Joyce Shala akitoa mafunzo kwa wadau wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) waliotembelea banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Hawa ni wananchi wanaojishughulisha na shughuli za kujiongezea kipato za kilimo wakisaidiwa na WFP. Katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka huu, DIB pia inashiriki huko Zanzibar na katika Kanda za Kaskazini jijini Arusha, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya na Kanda ya Mashariki mjini Morogoro.
Hata hivyo, Maonesho ya Nanenane Kitaifa yamefungwa Agosti 8,2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo kutokana na umuhimu wake ameongeza siku mbili ili washiriki waweze kutoa elimu na kuonesha huduma na bidhaa zao kwa wananchi wengi zaidi.
Tags
Bodi ya Bima ya Amana (DIB)
Deposit Insurance Board
(DIB)
Habari
Maonesho ya Nanenane
The Deposit Insurance Board (DIB)

.jpg)