NA ANNAMARIA BONDA
Ni moja ya asubuhi katika mwezi Juni, 2024 jua la wastani likichomoza kwa mwanga mdogo, mama mwenye umri wa makamo jina lake Bi. Riziki Shimba alikuwa ameketi kando ya kisima cha kienyeji kilichopo eneo la Senga, Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Alishika ndoo ya plastiki mkononi na kuitumbukiza kwa umakini kwenye kisima kifupi ambacho siku hiyo kilionekana kukauka maji mapema kuliko kawaida.
Moja ya eneo la utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 mjini Geita, utakaofanikisha huduma ya majisafi kwa wakazi kwa asilimia 100. Thamani ya mradi ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 53.463.“Tumekuwa tukipigia kelele huduma ya maji zaidi, kuweka kando jambo la dhahabu kwa miaka,” alisema huku akivuta pumzi ndefu ya uchovu. “Ni kweli Dhahabu inatufaidisha, lakini bila maji dhahabu hatuwezi kuiweka katika kiwango cha soko kama inavyohitajika.”
Kauli hiyo, iliyotamkwa na Riziki ya kutaka maendeleo na ongezeko la matumaini, imekuwa kama wimbo wa kisirisiri miongoni mwa wakazi wa Geita kwa muda mrefu. Mkoa huu, unaotajwa kuwa ni tajiri zaidi kwa uchimbaji wa madini nchini Tanzania, mojawapo dhahabu, mkoa wa Geita umekuwa na upungufu wa huduma ya majisafi na salama.
Lakini sasa hadithi hiyo imeanza kubadilika kwa namna isiyotarajiwa ikiwa ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Maji kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali.
Maneno na matarajio yaliyosubiriwa usiku na mchana, Serikali kupitia Wizara ya Maji imesimama kidete na kuleta mkombozi kama muarobaini wa huduma ya maji kwa wananchi: Mradi maarufu wa Miji 28. Kwa Geita, huu sio mradi tu wa maendeleo; huu ni kama mlango mpya wa kuingia katika zama za ustawi wa mji wa Geita na vitongoji vyake.
Mradi huu ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 11 Aprili 2023, ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 32, itakapofika mwezi Desemba 2025. Kwa takwimu, ujenzi wake tayari umefikia zaidi ya asilimia 64, ukisukumwa na nguvu ya pamoja ya wakandarasi ‘M/s Afcon Infrastructure Limited and Vijeta Project and Infrastructure Limited JV’ na mtaalamu mshauri WAPCOS Limited zilizoshinda kandarasi ya ujenzi, kampuni hizo zinatoka India, zikiwa na uzoefu tele wa kufikisha huuma yam aji katika jamii.
Lakini zaidi ya asilimia hizo za awali kuhusu Geita na maji, ni simulizi ya maisha ya kila siku kwa akina mama, watoto, wachimba wa dhahabu, wamiliki wa viwanda vya uchenjuaji na zaidi ya wananchi 700,000 wa kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Wananchi hawa na kazi zote hizo, sasa wanauona mradi huu wa Miji 28 kama mwangaza katika kona ya mwisho ya handaki.
Mradi huo unajumuisha ujenzi wa banio la maji (intake) chenye uwezo wa kupokea lita za maji milioni 46 kutoka Ziwa Victoria. Na si banio tu; pia kuna mtambo wa kuchakata na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 kwa siku. Takriban nusu ya lita bilioni moja kwa siku zitakuwa zinabubujika kutoka Ziwa Viktoria kukoleza uhai wa wakazi na kazi mbalimbali za Geita.
Katika maeneo ya Senga, Kaseni, Kagu, Geita Hill na Mpomvu, tayari matenki makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi mamilioni ya lita za maji na ujenzi wake umefika zaidi ya asilimia 95. Kwa uchache hatua hii inaleta picha gani kwa wananchi?
Ni kuondosha foleni ndefu za ndoo za plastiki kupata huduma ya maji. Hakuna tena kudamka usiku wa manane ili kuweza kuchota maji kabla kisima hakijakaushwa na jua. Hakuna tena kupoteza muda wa thamani ambao ungetumika kwenye kilimo, biashara au hata mahudhurio ya elimu kwa watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA), Mhandisi Frank Changawa, ndiye mtu aliyebeba dhamana nzito ya kuhakikisha mradi wa Miji 28 Geita unakamilika kwa wakati. Katika mahojiano anasema kwa sauti ya kujiamini:
“Geita inakua kwa kasi. Idadi ya watu inaongezeka, viwanda vipya vinafunguliwa kila siku, shughuli za uchumi zinakua kwa kuvuta watu wengi. miundombinu ya zamani haiwezi kukidhi mahitaji ya sasa. Hatuwezi kuendelea na hali hii bila kubadilika. Ukamilikaji wa mradi huu utaondoa uhaba wa maji kwa asilimia 100.”
Kauli hiyo ya Mhandisi Changawa haikuwa inajidhihirisha kwa macho kwa kumulika mji wa Geita. Ni ahadi iliyojengwa juu ya hesabu, utafiti na mipango ya muda mrefu ya Serikali, ikiwa ni sehemu ya malengo ya taifa ya kuhakikisha asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo Desemba 2025.

Katika pitapita za kila siku, ukizungumza na wakazi wa mji huo mitaani, hadithi kama ya Bw. Hassan Abdallah, mmiliki wa kiwanda cha uchenjuaji wa madini, ni ushahidi tosha wa athari chanya zinazotarajiwa. “Kuna wakati shughuli zinasimama kabisa,” Hassan anasema. “Uchenjuaji wa madini unategemea maji kwa asilimia 100. Bila maji, kila kitu kinasimama. Lakini sasa naona mwanga na siku mpya kabisa. Mradi huu ukikamilika, hangaika ya maji tutaisahau kabisa.”
Haiyumkini historia ya Geita si ya madini tu wala maji peke yake. Ni hadithi ya watu wenye subra, wasiokata tamaa na kusimama kila siku mpya kunapokucha kupigania maisha bora zaidi ya kunywa majisafi ya uhakika badala ya kuyatafuta kwa umbali mrefu au kutumia maji ya visima yasiyokuwa salama.
Maeneo kama Bugulula, Lahala, Kikwete, Kasota, Sungusila, Nyansalwa na Nyabalasana, vijana wa shule sasa wanatarajiwa kuanza kuhudhuria mafunzo ya shule kwa wakati bila kisingizio. Maji imekuwa sababu ya utoro au kuchelewa shuleni. Akina mama wengi nao wanatarajia kupata muda zaidi wa kuendesha biashara ndogo ndogo badala ya kutumia muda huo kuchota maji pia kujikita zaidi katika kazi nyingine za maendeleo.
Na kwa namna ya kipekee, wakazi wa Geita wanapenda kusema: “Tunatarajia kuondokana na uhaba wa huduma ya maji, kutokana na namna mradi unavyotekelezwa kwa kasi”, Bw. Hassan anasema.
Kauli hii, ambayo kwa mtu anayeisikia kwa mara ya kwanza huenda ikaonekana kama mzaha, ilhali mzizi wake unatokana na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya maji.
Ni tafsiri ya matarajio na ahueni ya hadithi za miaka mingi sasa zikigeuka kuwa halisi kwa uwekezaji mkubwa wa Serikali, uliojengwa na uhusiano mzuri wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na marafiki na nchi washirika wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa GEUWASA, Mhandisi Changawa mradi huu thamani yake ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 53.463.
Hata hivyo, kazi inayofanyika na Serikali thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha tu. Itapimwa na tabasamu za watoto watakaokuwa wakikimbia kwenda shuleni kwa wakati, tena bila madumu ya maji mkononi.
Inapimwa kwa mikutano ya wafanyabiashara wa Geita wanaojadili uwekezaji mpya na fursa lukuki zinazojiri, bila kuhofia viwanda kukosa maji. Inapimwa kwa kauli ya Mama Shimba anaposema kwa sauti ya furaha: “Muda si mrefu tunaenda kusahau kuhangaika kutafuta maji ya ziada kwa matumizi mbalimbali katika kazi zetu.”
Katika hotuba yake ya karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma za msingi kama maji zinawafikia wananchi wote, hasa katika maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi kama Geita. Na kweli, uamuzi wake wa kuwekeza katika miradi kama Mradi wa Miji 28 unaacha alama isiyofutika.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) wakati makala hii ikiandikwa, naye hakusita kuweka msisitizo: “Geita sasa haitakuwa tena mji wa dhahabu bila maji, utakuwa mji wa dhahabu na majisafi, salama na ya kutosheleza.”
Hadithi ya mji wa Geita, inafungua ukurasa mpya. Dhahabu bado ipo chini ya ardhi, lakini juu ya ardhi, maji yanatarajiwa kuwa tele nay a kutosha kwa kila kazi na kuwa chachu ya maendeleo zaidi.
Kweli, “Subira huvuta heri”. Na mji wa Geita umeonja matunda ya subira yake. Ni kama wakazi waliimba wimbo mmoja wa dini usemao “Usinipite, Mwokozi, Unisikie;
Unapozuru Wengine, Usinipite.. Bwana, Bwana, (naomba) Unisikie;
Unapozuru Wengini, Usinipite”. Serikali ya wananchi, nayo imesikia wimbo huo kutoka ka wakazi wa Geita na kuwekeza mradi wa maji wa miji 28 ili kuinua uchumi.