NA GODFREY NNKO
MATAIFA jirani yameendelea kuuamini Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS) nchini Tanzania kutokana na uimara na ufanisi wake.


Hayo yamesemwa leo Agosti 7,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon Mulokozi wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari nchini kupitia kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, mwenendo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja kuanzia mwaka 2021 hadi Septemba,2025 unaonesha mwitikio mzuri wa mataifa jirani kutumia mfumo huo na bandari za Tanzania, jambo ambalo ni la kujivunia kwani, wangeweza kutumia Bandari za Msumbiji au Kenya.
Amesema, mwaka 2021 licha ya changamoto ya UVIKO-19, mataifa jirani yalitumia mfumo huo kuagiza mafuta zaidi ya tani milioni 2. Huku kwa matumizi ya ndani ya nchi ikiwa tani milioni 3. Katika, mwaka huo, mfumo huo uliagiza na kuingiza mafuta zaidi ya tani milioni 5.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, kwa mwaka 2022,mfumo huo uliagiza mafuta zaidi ya tani milioni 6 huku tani zaidi ya milioni 3 zikipelekwa mataifa jirani na tani milioni zaidi ya 2 zikibaki nchini kwa ajili ya matumizi.
Aidha, mwaka 2023 amesema, mfumo huo uliagiza mafuta tani zaidi ya milioni 5 huku zaidi ya tani milioni 2 zikitumika ndani ya nchi na nyingine zaidi ya milioni 2 zikipelekwa mataifa jirani.
Mwaka 2024 amesema kuwa, mfumo huo uliagiza mafuta zaidi ya tani milioni 6 huku tani milioni 3 zikiwa kwa ajili ya matumizi ya ndani na tani zaidi ya milioni 3 zikipelekwa mataifa jirani.
Aidha, mwezi Januari hadi Septemba, 2025 amesema, mfumo huo uliagiza mafuta tani zaidi ya milioni 5 huku tani milioni 3 zikipelekwa mataifa jirani na tani milioni zaidi 2 zimetumika nchini.
Mulokozi amefafanua kuwa, mwelekeo unaonesha kuwa, hadi kufikia Desemba, mwaka huu wa 2025 kuna matarajio makubwa ya kuongezeka kiwango cha uagizaji mafuta.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri, akizungumza wakati wa mkutano na Wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam, Agosti 7, 2025.
Amesema, ongezeko hilo si tu kwamba litasaidia katika huduma ya mafuta nchini, pia ni nyenzo muhimu ya kufungua fursa za ajira kwa Watanzania katika idara mbalimbali.
Lakini, vilevile katika kujifunza, nchi zote zinazotuzunguka amesema, zimekuwa zikija kujifunza kuhusu mfumo huo ikiwemo Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi na nyinginezo.
"Hata Kenya wanakuja kujifunza kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja, kwa hiyo Mlmfumo unaendelea kuimarika na unaendelea kuaminikana na nchi jirani katika uagizaji wa mafuta kupitia bandari za Tanzania."
Amesma, lengo la Serikali la kuanzisha taasisi husika ni kuhakikisha nchi inapata nishati ya mafuta ya uhakika.
Katika hatua nyingine, Bw.Mulokozi amesema kuwa, uwekezaji katika maghala ya kuhifadhi mafuta nchini umeongezeka kutoka maghala 22 mwaka 2021 hadi 24 mwaka 2025.
"Na uwezo wa kuhifadhi umeongezeka kutoka lita milioni 1,288.101 hadi lita milioni 1,721.327,"amefafanua Mulokozi.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 34 likichochewa zaidi na upanuzi mkubwa wa maghala.
TR
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Sabato Kosuri amesema, Msajili wa Hazina anatambua na kuthamini kazi nzuri inayofanywa na wanahabari nchini huku akiwahimiza kuendelea kutumia kalamu zao kupasha habari zinazowaunganisha Watanzania na kudumisha uzalendo.

"Msajili wa Hazina amewapongeza kwa juhudi na ushirikiano ambao mmekuwa mkitupa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Serikali kwa ujumla."
Bw.Kosuri amesema, Msajili wa Hazina, Bw.Nehemiah Kyando Mchechu ataendelea kutoa kipaumbele kwa mikutano na vyombo vya habari ili taasisi na mashirika ambayo yapo chini ya ofisi yake ziweze kuelezea masuala mbalimbali.
Pia, amesema kuwa, ataendelea kutoa ushirikiano yeye kama Msajili wa Hazina na mashirika ya umma ambayo anayasimamia ili kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na vyombo vya habari nchini.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Kikao Kazi Msajili wa Hazina
Ofisi ya Msajili wa Hazina
PPBPA
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)