Minara 661 kati ya 758 yaanza kutoa huduma kwa wananchi

DODOMA-Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea kutekeleza kwa mafanikio mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, hii ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi waishio maeneo ya vijijini wanapata huduma bora za mawasiliano ya simu na intaneti.
Hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2025, jumla ya minara 661 kati ya hiyo 758 imekamilika na tayari imeanza kutoa huduma kwa wananchi, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia asilimia 87.20.

Ujenzi wa minara hii ni sehemu ya mkakati wa kupunguza pengo la mawasiliano kati ya maeneo ya mijini na vijijini, na kuongeza fursa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wote.

Wananchi katika maeneo ambako minara imekamilika wameripoti maboresho makubwa ya huduma za mawasiliano, hali inayorahisisha shughuli za kila siku kama vile biashara, elimu kwa njia ya mtandao, huduma za kifedha, na upatikanaji wa taarifa muhimu.

Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na kampuni za mawasiliano nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kujenga uchumi wa kidijitali na kuhakikisha hakuna mtanzania anayebaki nyuma katika zama za TEHAMA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news