DAR-Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wazalishaji wa maudhui mitandaoni kuchukua tahadhari kuhusu matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) hususani katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu ili kuepuka taarifa za upotoshaji ambazo zinaweza kuwagawa wananchi na kuvuruga amani nchini.
INEC ina wajibu wa kusimamia na kuratibu uendeshaji wa chaguzi kwa mujibu wa sheria ili kulinda demokrasia kwa manufaa ya wananchi, vyama vya siasa na wagombea nchini Tanzania.
Rai hiyo imetolewa leo Agosti 3,2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Jacobs Mwambegele katika mkutano wa Kitaifa kati ya tume na wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
"Nawasisitiza na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya Akili Unde ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza habari za upotoshaji hasa kupitia mitandao ya kijamii."
Pia, Jaji Mwambegele amewataka wazalishaji maudhui hao kuhakikisha taarifa zinazopandishwa katika majukwaa yao zinakuwa za kweli na zisizo na chembe ya upotoshaji ili kupeuka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema kuwa, tume hiyo ina matumaini makubwa na vyombo vya habari katika kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu kupitia ushiriki wao nchini.
Amesema, imani hiyo inatokana na ushirikiano wa vyombo vya habari waliouonesha tangu awali kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga nchini.
"Na mmekuwa wepesi wa kuwasilisha hoja na ushauri pale inapohitajika kila tunapokutana nanyi kwenye vikao," amesisitiza Jaji Mwambegele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema, tume mejiwekea utaratibu wa kuvishirikisha vyombo vya habari katika mchakato mzima wa uendeshaji wa uchaguzi ili kuweka uwazi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
Kailima ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na ushiriki wa vyombo vya habari katika mkutano huo wa waandaaji wa maudhui mitandaoni.
Amesema, tume inatarajia vyombo vya habari na wanahabari watatumia kalamu zao na nyenzo walizonazo kuhubiri amani katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
"Tunawaomba na kuwasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi, "amesema Kailima.
Aidha, kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni Kura Yako, Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura.
