DAR-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ameipongeza kampuni ya SportPesa na Klabu ya Yanga kwa kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu, akisisitiza kuwa mchango wa wadhamini kutoka sekta binafsi ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya michezo nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba mpya wa udhamini wenye thamani ya Shilingi Bilioni 21.75 kati ya Yanga na SportPesa, Mhe. Mwinjuma amewapongeza kwa kudumu kama washirika kwa miaka nane ambapo udhamini umekuwa na tija sio tu kwa klabu hiyo, bali pia ustawi wa michezo kwa ujumla."Najua Rais wa Yanga alisema lengo ni kuvuka hatua ya makundi, lakini ninaamini anawaza mbali zaidi ikiwemo kuona Yanga inatwaa ubingwa wa Afrika. SportPesa mmeona uwezo huo na mmeamua kuwekeza. Huu ni mfano bora wa sekta binafsi kusaidia kufikia malengo ya michezo nchini," amesema Mwinjuma.
Amefafanua kuwa ushirikiano wa SportPesa na Yanga unaendana na Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na Sheria Na. 12 ya Baraza la Michezo la Taifa, ambazo zote zinatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuendeleza michezo.
Aidha,Mhe.Mwinjuma amebainisha kuwa michezo huchangia si burudani pekee bali pia maendeleo ya kiuchumi, kukuza afya za Watanzania, na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza hivyo amesema serikali inaendelea kuhakikisha mazingira rafiki kwa wawekezaji na wadhamini wa michezo ili kuvutia uwekezaji zaidi katika vilabu na mashindano."Tunataka kuendelea kuwa na makampuni mengi kama SportPesa, benki, na mashirika mengine ambayo yanaona fursa katika michezo yetu. Huu ni uwekezaji ambao mmepata faida nao na mmewasaidia wachezaji na klabu kukua," ameongeza.
Amemalizia kwa kusisitiza kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana na wadhamini wote kuhakikisha michezo inakua na kufikia viwango vya kimataifa.















