Michezo ya kubahatisha si mbadala wa ajira ni burudani na haipaswi kupitiliza-GBT

NA GODFREY NNKO

BODI ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) imesema kuwa, michezo ya kubahatisha si mbadala wa ajira badala yake ni sehemu ya burudani kwa wanaocheza na burudani hiyo haipaswi kupitiliza.
"Michezo ya kubahatisha ni sehemu nyingine ambayo imeongeza wigo wa burudani, kwa hiyo inapaswa kuwa sehemu ya burudani kwa wanaocheza na si kazi, hii ni bahati, kwani kwenye michezo hii hakuna ufundi wowote wa kucheza."

Mkurugenzi wa Huduma wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. Daniel ole Sumayan ameyasema hayo leo Agosti 12,2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kikao hicho ni mahususi kwa ajili ya kuelezea mafanikio ya taasisi hiyo ya umma katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Bw.Sumayan amesema, kwa vile hii ni burudani kila mmoja anapaswa kuburudika kwa kiasi ili kuepuka uraibu ambao unaweza kusababisha kero badala ya furaha katika jamii na kiuchumi.

GBT ni taasisi ya umma iliyoanzishwa Julai Mosi,2003 kwa Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Na.4 ya mwaka 2003.

Miongoni mwa majukumu ya taasisi hii ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha huku ikiwa chini ya uangalizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuratibu na kudhibiti uendeshaji wa michezo ya kubahatisha nchini.

Mkurugenzi wa Huduma wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw.Daniel ole Sumayan amesema, sekta ya michezo ya kubahatisha hapa nchini bado ni changa ingawa inaendelea kukuwa kutokana na jamii kuendelea kuikubali.

Amesema kuwa, michezo ya kubahatisha imegawanyika katika makundi mawili ikiwemo michezo ya kibiashara na ambayo si ya kibiashara.
Kwa upande wa michezo ya kibiashara amesema kuwa,huendeshwa na kampuni zilizosajiliwa na kupewa leseni na GBT ambapo ulipa kodi.

Miongoni mwa michezo hiyo inajumuisha ile ya majumba maalum na mitandaoni (Cassino), mashine za sloti ambayo huchezwa katika maduka maalum na baa.

Pia, amesema kuwa, kuna ubashiri wa matokeo ya michezo kwenye mitandao na maduka na bahati nasibu ya jumbe fupi za simu. Nyingine ni maduka ya mashine ya arubani na Bahati Nasibu ya Taifa nchini.

Aidha, kwa upande wa michezo isiyokuwa ya kibiashara amesema, huwa inafanyika kwa vipindi vifupi na huendeshwa na kampuni zinazofanya biashara ya bidhaa au huduma mbalimbali ili kukuza biashara zao.

Sambamba na vikundi vya jamii vyenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya malengo maalum.

"Ni kinyume cha sheria kuendesha michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT). Utoaji wa leseni za michezo ya kubahatisha ni mchakato unaohusisha uchunguzi wa kina kwa muombaji ili kubaini iwapo ana sifa stahiki."
Bw.Sumayan amesema, mambo yanayochunguzwa yanajumisha historia ya kiuhalifu, chanzo cha fedha, uwezo wa muombaji kifedha, kiteknolojia na kitaalamu.

Vilevile, uchunguzi huo huwa unaangazia washirika wa biashara ikiwemo usafi, uadilifu, uaminifu wao na utii wa sheria.

Amesema, leseni hizo utolewa na bodi ndani ya mwaka mmoja na itahuhishwa iwapo mtoa huduma hiyo ataendelea kukidhi sifa za kuwa mtu safi.

Pia, amesema, michezo ya kubahatisha haipaswi kuwa karibu na nyumba za ibada, shule na ili eneo liweze kuruhusiwa lazima lifanyiwe ukaguzi na wataalamu kutoka bodi.

Wakati huo huo, amesema kuwa, michezo ya kubahatisha nchini imekuwa na michango chanya, kwani kodi ya michezo ya kubahatisha iliongezeka kutoka shilingi bilioni 131.99 kwa mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 260.21 mwaka 2024/25.
Ofisi ya Msajili wa Hazina

Awali,Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Sabato Kosuri amesema kuwa,mikutano hii imekuwa daraja muhimu kati ya taasisi, mashirika ya umma na vyombo vya habari nchini.

Pia,amesema kupitia mikutano hii, tangu ianze umma umekuwa ukipata elimu na kuyafahamu mambo mbalimbali yanayoendelea katika taasisi hizo ambazo ni mali yao na mafanikio yaliyopatikana.
Bw.Sabato amesisitiza kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kuratibu mikutano hii ili kuhakikisha kuwa kila taasisi inashiriki ziweze kuelezea walipotoka, walipo, wanapoelekea na mafanikio yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news