Rais Dkt.Mwinyi aishukuru Qatar kwa kuunga mkono miradi ya maendeleo Zanzibar



ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kiuchumi katika sekta mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 10.
Hafla hiyo imefanyika leo Agosti 29,2025 Ikulu,Zanzibar ambapo kwa upande wa Qatar mkataba huo ulisainiwa na mmoja wa Wanafamilia ya Kifalme wa Qatar, Mhe.Sheikh Mansour Bin Jabor Bin Jassim Al Thani, ambaye pia ni Mmiliki wa Kampuni ya Al Mansour Holding itakayotekeleza miradi hiyo.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, utiaji saini uliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Ndg. Khamis Mwalim Suleiman.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Qatar kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Zanzibar katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayohitaji uwekezaji mkubwa.
Rais Dkt. Mwinyi ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uhifadhi wa mafuta, ujenzi wa kumbi za mikutano, ujenzi wa bandari, utalii, uchumi wa buluu na nishati ya umeme.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameuelezea mkataba huo kuwa ni hatua ya kufariji, akibainisha kuwa miradi hiyo imepata wawekezaji wenye dhamira na uwezo mkubwa wa kifedha kutoka nje ya nchi.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga vema kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa miradi hiyo, ambayo ameeleza kuwa itaongeza ushirikiano wa muda mrefu baina ya Qatar na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news