JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa kutokana na uongozi wa kipekee wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Jumatano, Agosti 13, 2025, Rais Samia alitunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima ya Maji “Presidential Global Water Changemakers Award 2025”, heshima ya kipekee iliyotolewa na Global Water Partnerships kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika.
Tuzo hiyo, iliyokabidhiwa na Rais Duma Boko wa Botswana, Mwenyekiti wa Tuzo hizi, ilipokelewa kwa niaba ya Tanzania na Balozi James Bwana nchini Afrika Kusini. Tuzo hii ilitolewa wakati wa Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji Barani Afrika unaoendelea jijini Cape Town na utahitimishwa Agosti 15, 2025.
Katika kutambua mchango wa Rais Samia, yafuatayo yameelezwa:
■Upanuzi wa miundombinu ya maji na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi nchini Tanzania.
■Ubunifu wa kifedha, ikiwemo utoaji wa Hati Fungani ya Kijani (Green Bond) kupitia Mamlaka ya Maji Tanga, ili kuhakikisha miradi ya maji inapata fedha endelevu.
■Mageuzi ya kistratejia yaliyoimarisha utawala na ufanisi katika sekta ya maji.
Rais Samia amesimama bega kwa bega na viongozi wengine mashuhuri waliotunukiwa tuzo hii, wakiwemo Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan wa UAE, Mwanaufalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia, na Mfalme Letsie III wa Lesotho.
Tuzo hii ni ushuhuda wa uongozi wa matokeo wa Rais Samia na dhamira yake ya maendeleo endelevu nchini Tanzania. Inathibitisha kwamba uongozi wa kimaendeleo, ubunifu, na kujituma kwa wananchi unaweza kuleta mabadiliko halisi na kuvutia heshima ya dunia nzima.
Chini ya uongozi wake, Tanzania inaendelea kung’ara kimataifa, ikionyesha kuwa uongozi wa kina mama Samia ni wa matokeo, unaojali wananchi, na unaoongozwa na maono ya maendeleo.
