NA LWAGA MWAMBANDE
NI wazi kuwa,kila mtu anawajibika kutenda haki mahali alipo, na tunapaswa kuwatendea haki tunaoishi nao, tunaowaongoza na tunaokutana nao popote tunapokuwa katika jamii.
Kwa mujibu wa wakili Isaack Zake anabainisha kuwa,neno Haki kwa tafsiri ya kamusi ya Kiswahili sanifu lina maana ya jambo ambalo mtu anastahiki au kitu anachostahili kuwa nacho.
Kwa tafsiri ya kamusi ya kisheria neno Haki lina maana ‘kile mtu anachostahili kuwa nacho au kile anachoruhusiwa kufanya, au kile anachostahili kupokea kutoka kwa wengine kwa mujibu wa sheria’.
Kwa tafsiri hii tunaweza kuona kuwa sheria ndio msingi wa haki, sheria ndio inasema kile unachostahili kuwa nacho au unachoruhusiwa kufanya au unachotakiwa kupata kutoka kwa wengine. Kwa maana pana zaidi tunaweza kusema Haki ni maslahi ya mtu ambayo yanatambuliwa na kulindwa na sheria.
Ukirejea katika neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kitabu cha Mithali 14:34 neno linasema kuwa “Haki huinua Taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wote.”
Vilevile,Mithali 15:6 neno la Mungu linasisitiza kuwa,katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi, bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.
Mfalme Hezekia alipougua na akiwa katika hofu ya kufa, kilichomponya ni kazi alizofanya kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Rejea Isaya 38:1-7...."Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.
"Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA, akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako.
"Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.
"Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu."
Aidha, 2 Wathesalonike 3:13 neno la Mungu linasema "Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema." na Waefeso 5:8-11 inasema "Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee".
Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,kutenda haki ni nguzo muhimu katika kuinua Taifa. Endelea,
¹Kujitenga na uovu, ni njia ya mwenye haki,
Kukumbatia uovu, njia ya asiye haki,
Ni vema tena werevu, kuikumbatia haki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
²Hauishi uonevu, kama unatenda haki,
Na hata ule uvivu, hapo haukamatiki,
Hapo utashi na nguvu, ndivyo vinapamiliki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
³Kwanza Mungu kumpenda, ilo lazima hakiki,
Kote kule unakwenda, kwako iwe ndiyo kiki,
Kwa yote kutakulinda, usifanye unafiki,
Hebu inua tafa, kwa kuwa mtenda haki.
⁴Mungu kama wampenda, huwezi kuwa na chuki,
Wengine ukawaponda, wabakie tikitiki,
Neno lake takufunda, uweze kuwabariki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
⁵Jinsi alivyojitoa, aweze kutumiliki,
Mauti kuiondoa, kufa hatumaliziki,
Akufanye kujitoa, kufanya yaliyo haki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
⁶Ni Mungu atuagiza, jirani kuwa rafiki,
Yale yanatupendeza, kwao tusiyataliki,
Hiyo ninakueleza, inaendana na haki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
⁷Mambo ya kusingizia, hayo ni kosa si tiki,
Wengine kufanyizia, kwako hayumkiniki,
Utakavyojifanyia, na wengine wabariki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
⁸Endapo hutendi haki, kipimio haufiki,
Kwenye taifa ni dhiki, wala hapo hubariki,
Tutaona hatufiki, kumbe wewe mzandiki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
⁹Haki inapokanyagwa, alama hatuandiki,
Tusiseme tumerogwa, na kuwapa watu chiki,
Ni wenyewe tunapigwa, twendako hakuendeki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
¹⁰Ni nini mchango wako, katika kutenda haki,
Ujichunguze uliko, ni mkweli au feki,
Basi usibaki huko, ufanye tukulaiki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
¹¹Jirani yako mpende, acha wote unafiki,
Mema kwake uyatende, uje nawe tukulaki,
Acha ngazi uzipande, utawale umiliki,
Hebu inua taifa, kwa kuwa mtenda haki.
(Mithali 16:17, 14:34, Marko 12:30)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
