Sekta ya kilimo yatajwa kuwa nyenzo muhimu Zanzibar

ZANZIBAR-Sekta ya kilimo imeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu inayoweza kuwasaidia vijana kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar (BAVIZA), Ali Haji Hassan, wakati wa ziara ya kimasomo kwa vijana wa mabaraza ya vijana katika Shamba la Mfikiwa Cooperative, lililopo Mfikiwa, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Katibu Mtendaji amewahimiza vijana kutumia vyema fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo na kuwa wabunifu ili kujiendeleza kimaisha. Amesema ubunifu na moyo wa kujitolea ni nyenzo zitakazosaidia vijana kufanikisha malengo yao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Niwaambie vijana tuitumie vyema fursa hii ya kilimo ili tuweze kutatua changamoto zetu za ajira. Kilimo sasa ni fursa na utajiri unaokuwezesha hata wewe kuwaajiri wengine,”amesema Katibu huyo.

Aidha, amewapongeza viongozi wa Mfikiwa Cooperative kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuonesha kuwa kilimo ni ajira yenye tija endapo itafanywa kwa bidii na maarifa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mfikiwa Cooperative Society, Abdulhalim Said Suleiman, amesema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 14 lilianzishwa mwaka 2002 na linazalisha matunda, mboga mboga, mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kuku.

Kwa sasa, shamba hilo lina wafanyakazi wa kudumu 16 na wa muda mfupi 8, huku likifanikiwa kufanya biashara na taasisi mbalimbali na kuzalisha ndizi aina ya Kimalindi zinazojulikana kwa ustahimilivu wa hali ya hewa. Bidhaa zake zinauzwa katika Kisiwa cha Pemba, na mipango ipo ya kupanua soko hadi Unguja.

Akizungumza kwa niaba ya vijana walioshiriki, Fahad Ismail Khamis amesema ziara hiyo imewafumbua macho na kuwapa maarifa ya namna kilimo kinavyoweza kuwa chanzo cha ajira na maendeleo, huku akiahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa vitendo.

Ziara hiyo ya mafunzo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, yatakayofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Utaani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news