Vijana Zanzibar watakiwa kuchangamkia fursa

ZANZIBAR-Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe.Salama Mbarouk Khatib amesema, Serikali itaendelea kutoa fursa mbalimbali kwa vijana katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, na amewataka vijana kuzichangamkia ili kujiletea maendeleo.
Ametoa kauli hiyo katika Kongamano la Kitaifa la Vijana lililofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Utaani, Wilaya ya Wete, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa 2025.

Mhe. Salama amesema,wakati umefika kwa vijana kujitambua na kutumia nafasi zilizopo kuunga mkono jitihada za Serikali na sekta binafsi, hatua itakayowasaidia kupunguza changamoto ikiwemo ukosefu wa ajira.
"Changamoto mlizonazo mzitazame kama fursa ya kuifikia ndoto zenu. Kuwa na mwamko wa kuzitengeneza fursa kupitia changamoto hizo," amesisitiza.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zao za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mhe. Salama amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kulinda amani kabla na baada ya uchaguzi.

"Nawaasa vijana musikubali kwa namna yoyote ile kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa maslahi yao binafsi na kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani,"ameonya.

Pia amezipongeza Idara ya Maendeleo ya Vijana na Baraza la Vijana Zanzibar kwa mchango wao katika kutatua changamoto na kuendeleza ustawi wa vijana kupitia maendeleo ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mfamau Lali Mfamau, amewahimiza vijana kutumia maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kujitathmini na kuangalia mchango wao kwa taifa.

Kongamano la siku moja hilo limewashirikisha vijana na taasisi mbalimbali kutoka Unguja na Pemba likibeba kaulimbiu ya Siku ya Vijana Kimataifa 2025: “Wakati wangu ni sasa, nitashiriki kuchagua na kuchaguliwa kwa maendeleo endelevu.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news