SELF Microfinance Fund yahimiza mikopo itumike kwa malengo

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund) umewataka wanufaika wa mikopo mbalimbali nchini kuendelea kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuwapa matokeo bora katika uzalishaji.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF, Bi. Santieli Yona ameyasema hayo leo Agosti 15,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Sisi tunashauri, kabla ya kwenda kukopa, ni vizuri ukafanya tathmini ya kina ya kile ambacho unataka kuzalisha, ili baada ya kupata mkopo uweze kufanya kile ambacho umekusudia kwa ufanisi. Na ujue kabisa unapaswa kuulipa huo mkopo, baada ya kukopa.

"Unapotumia mikopo vizuri, uwe na uhakika utakusaidia, lakini unapotumia bila malengo mkopo unaweza kukuingiza katika matatizo,"amesisitiza Bi.Yona.
"Sisi, SELF Microfinance tutaendelea kuwapa watu fursa ya kufanya shughuli za kuzalisha mali na kutoa huduma ndogo za fedha, huu ni mfuko, lakini pia ni taasisi inayofanya kazi chini ya Wizara ya Fedha."

Amesema, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Juni,2025 chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, wamewezesha kupatikana ajira zaidi ya 1830,000 kupitia wakopaji na wakopeshaji wanaopata huduma kutoka taasisi hiyo hapa nchini.
Amesema, kwa hivi karibuni wameanza kutoa mikopo ya nishati safi ya kupikia ambayo lengo lake ni kusaidia watu ili kutumia nishati rafiki ambayo itaepusha uharibifu wa mazingira.

Mbali na mikopo ya nishati safi, Bi.Yona amesema kuwa, mfuko huo unatoa mikopo ya watumishi wa umma, wafanyabisahara, wajasiriamali wadogo na wa kati, mikopo ya wakulima na mkopo wa wazabuni.

Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Juni, 2025 amesema,mikopo iliyotolewa na taasisi kwa makundi mbalimbali inafikia zaidi ya shilingi bilioni 190 huku mikopo chechefu ikiwa chini ya asilimia 10.
"Sisi kama taasisi, tunatoa pia huduma za bima, kuhakikisha inalinda mikopo ambayo tunatoa,"amesisitiza Bi.Yona ambapo amesema kuwa, kwa sasa wana matawi 12 nchini ambayo yanatoa huduma kila mkoa na wanatarajia kuiongeza matawi hadi kufikia 20.

Pia, ameishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuja na wazo la taasisi na mashirika ya umma kuleta kile wanachokifanya mbele ya umma ili wananchi waweze kutambua huduma, mafanikio na mwelekeo wa taasisi hizo.



Mfuko wa SELF (SELF MF) ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo kwa wananchi hasa wa kipato cha chini wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza umasikini.
Mfuko wa SELF ulianza kutekeleza majukumu yake tarehe Mosi Julai, 2015, ukirithi majukumu ya Mradi wa Serikali uliojulikana kama “Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF) Project. Mradi ulitekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.

Ofisi ya Msajili wa Hazina

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Sabato Kosuri amesema kuwa, mikutano hii ni daraja na fursa kubwa kwao kama taasisi na mashirika ya umma katika kushauriana ili kuboresha na kuimarisha utendaji wa kazi kwa ustawi wa taasisi husika na Taifa kwa ujuma.
Bw.Sabato amesema kuwa, mikutano hii wanaichukulia kama kioo ambapo dhamira na nia ni kuwezesha kila mmoja aliyekasimiwa majukumu katika taasisi au shirika la umma anafanya vema zaidi kwa matokeo bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news