Serikali inaendelea kusimamia ujenzi wa uwanja mkubwa wa AFCON na miundombinu mbalimbali inayojengwa Fumba-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa uwanja wa AFCON.
Sambamba na miundombinu mbalimbali inayojengwa Fumba, hivyo ni muhimu kubaini mapema maeneo yatakayotumika kwa mradi huo ili kuepusha mwingiliano wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo kati ya taasisi husika.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 11,2025 Ikulu,Zanzibar katika kikao maalum na mawaziri mbalimbali akiwemo Mhe.Rahma Kassim Ali, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Mhe. Shariff Ali Shariff, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji,
Mhe. Tabia Maulid Mwita, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, pamoja na Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB), kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu matumizi sahihi ya ardhi katika maeneo ya uwekezaji Fumba.
Mara baada ya kikao hicho, Rais Dkt. Mwinyi aliridhia mapendekezo yaliyoafikiwa katika kikao hicho ya kutembelea maeneo husika ya Fumba, ili kupata uhalisia wa miradi hiyo pamoja na mtandao wa barabara, hatua itakayosaidia kupanga utekelezaji kwa ufanisi na kuondoa changamoto za upangaji wa ardhi.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi pia alitembelea eneo linaloendelea kujengwa viwanja vya michezo vitakavyotumika kwa michuano ya AFCON 2027.
Akihitimisha ziara yake, Rais Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuzungumza na wakaazi wa Kisakasaka ambao wametoa maeneo yao kupisha ujenzi wa Ofisi za Serikali na jengo la Baraza la Wawakilishi.

Amewahakikishia kuwa Serikali itawafidia ardhi zao kwa fedha au nyumba za makaazi, kulingana na ridhaa ya kila mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news