NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan umeendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira ambapo kupitia soko la bima, ajira rasmi zimeongezeka kutoka wafanyakazi 3,527 mwaka 2021 hadi kufikia wafanyakazi 6,916 mwishoni mwa Juni,2025.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 96.1 ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 18.3 za ajira kwa mwaka katika soko la bima nchini.
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware ameyasema hayo leo Agosti 18,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Dkt.Saqware amesema, mafanikio hayo hayakuja kwa bahati bali ni kutokana na utekelezaji wa Sera nzuri chini ya uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia.Vilevile, amesema mali za bima na thamani ya mali katika soko la bima imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.28 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 2.34 mwaka 2024 sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 83.3.
Amesema,ukuaji huo ni wastani wa ongezeko la asilimia 16.3 kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2025 kwa maana ya Januari na Juni, thamani ya mali katika soko la bima iliongezeka kutoka shilingi trilioni 2.34 mwishoni mwa mwaka 2024 hadi kufikia shilingi trilioni 2.49 kufikia Juni 30,2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.6.
Pia,amesema thamani ya mitaji katika soko la bima imeimarika kutoka shilingi bilioni 416.0 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 847.3 mwaka 2024 sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 103.7, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 26.3 kwa mwaka.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, Dkt.Baghayo Saqware amesema, thamani ya mitaji katika soko la bima iliongezeka kutoka shilingi bilioni 906 mwaka 2024 hadi bilioni 993 kufikia Juni 30, 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.5.
Mbali na hayo, Dkt.Saqware akizungumzia kuhusu uandikishaji wa ada za bima katika soko la bima nchini amesema,umeongezeka kutoka shilingi bilioni 911.5 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 1.418 mwaka 2024.
Amesema,hilo ni sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 55.6 katika kipindi cha miaka minne ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 11.7 kwa mwaka.
Vilevile, katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2025, Dkt.Saqware amesema, uandikishaji wa ada za bima umefikia shilingi bilioni 831.8.
Pia, amesema katika kipindi hicho mchango wa bima katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 2.01 mwaka 2023 na unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia tatu ifikapo mwaka 2030.
Dkt.Saqware amesema,katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, kumekuwa na ongezeko la bidhaa mpya za bima, ambapo kwa wastani bidhaa 15 mpya zimekuwa zikipewa idhini na mamlaka kila mwaka kwa ajili ya kuuzwa katika soko la bima nchini.
Amesema,katika kipindi cha Januari hadi Juni 2025, jumla ya bidhaa 10 mpya za bima zimepewa idhini na namlaka kuingia sokoni zikiwemo bidhaa za bima za kilimo na ufugaji.
Dkt.Saqware amefafanua kuwa,kiwango cha ubakizaji bima nchini kwa bima za kawaida kimeongezeka kutoka asilimia 55.9 mwaka 2021 hadi asilimia 58.5 mwaka 2024.
Aidha, kiwango cha ubakizaji bima kwa bima za maisha kimeongezeka pia kutoka asilimia 85.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 86.2 mwaka 2024;
Dkt.Saqware amesema, pia ulipaji wa madai ya bima umeongezeka kutoka shilingi bilioni 397.6 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 592.1 mwaka 2024 sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 48.9 katika kipindi cha miaka minne ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 10.5 kwa mwaka.
Aidha, wastani wa muda unaotumika na kampuni za bima kulipa madai ya bima yasiyo na utata umeimarika kutoka wastani wa siku 73 hadi ndani ya wastani wa siku 45.
Kuhusu mchango wa Sekta ya bima kwenye mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Kampuni (corporate tax) pekee, umeongezeka kutoka shilingi bilioni 137.7 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi bilioni 183.1 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 32.97.
Wakati huo huo, wakati wa uwasilishaji wa taarifa hiyo, Dkt. Saqware amewahimiza wahariri na vyombo vya habari kwa ujumla kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo.
Amesema kuwa,vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee ya kuwa daraja kati ya sekta ya bima na wananchi, na hivyo vina jukumu la kuhakikisha elimu ya bima inawafikia Watanzania wote kwa njia mbalimbali.
“Wanahabari mnapaswa kuwa wasemaji wabobezi wa masuala ya bima ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na zenye kuaminika."
Amesema,kupitia kalamu na majukwaa yao mbalimbali wananchi wataweza kuelewa nafasi ya bima katika maisha yao.
Kuhusu TIRA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), chini ya Sheria ya Bima, Sura ya 394 ina jukumu la kuendeleza sekta ya bima Tanzania Bara na Zanzibar.
Pia, ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha na uangalizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo ilianzishwa ili kutekeleza majukumu ya kusimamia soko na kuendeleza biashara ya bima nchini na masuala yanayohusiana na bima kwa mujibu wa sheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu mengine ni kusajili kampuni za bima nchini, kusimamia na kukagua mwenendo wa kampuni za bima nchini, kutoa elimu ya bima kwa umma, kuhakikisha uendelevu, uhimilivu na usalama wa soko la bima nchini. Vilevile, kuishauri Serikali kuhusu masuala ya bima hapa nchini.
Tags
Habari
Kikao Kazi Msajili wa Hazina
Kikao kazi na Wahariri
Ofisi ya Msajili wa Hazina
TIRA
TIRA Tanzania
