Tanzania kuingia katika ramani ya Kimataifa ya Utalii wa Mikutano (MICE)

DAR-Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta ya Utalii wa Mikutano, Maonesho, Makongamano na Safari za Motisha (MICE) kama njia mpya ya kukuza uchumi, kuongeza ajira, na kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Akizungumza katika Jukwaa la Wadau wa Sekta ya MICE lililofanyika jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena, Ernest Mwamaja aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alieleza dhamira ya serikali kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mikutano barani Afrika.

“Serikali imeshaweka wazi kuwa utalii wa mikutano ni zao la kibiashara ambalo lina nafasi kubwa ya kuongeza mapato ya taifa na kuchochea shughuli za kiuchumi,” amesema Mwamaja.
Amefafanua kuwa, kuingia rasmi katika sekta hii kutaiweka Tanzania kwenye ramani ya mataifa yanayofaidika na aina hiyo ya utalii, na pia kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi kwa shughuli za kibiashara na vikao.

Katika tukio hilo, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliwasilisha tathmini ya mwenendo wa sekta ya MICE nchini, ikiwa ni pamoja na changamoto na fursa zilizopo. Miongoni mwa maendeleo yaliyotajwa ni ujenzi wa ukumbi mpya wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 5,000 jijini Arusha, hatua inayolenga kuvutia mikutano ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mariam Ndabagenga, Mkurugenzi wa taasisi ya Popular Links inayojihusisha na utalii wa mikutano, alibainisha kuwa Tanzania ina kila kitu kinachohitajika kuifanya kuwa kitovu cha MICE Afrika.

“Tanzania ina rasilimali nyingi, miundombinu mizuri, hoteli za kisasa, vivutio vya asili na watu wenye ujuzi wa kuandaa matukio makubwa. Tunahitaji sasa kuweka mfumo rasmi wa uratibu na chombo maalum cha kusimamia sekta hii,” alisema Mariam.

Aidha, aliongeza kuwa kuna haja ya kuhakikisha wageni wanaokuja kwa mikutano wanafikiwa na huduma bora ili wachangie zaidi katika uchumi na kushawishika kurudi tena.

“Wageni wanaokuja kwa ajili ya mikutano huwa na uwezo mkubwa kifedha. Wanahitaji huduma bora, na wakiridhika huleta wageni wengine. Ni muhimu kuhakikisha hawabaki tu Dar es Salaam, bali wanafika kwenye vivutio vyetu vya utalii,” alieleza.
"Tofauti na aina nyingine za utalii, utalii wa mikutano hauna misimu maalum, hivyo unasaidia kuleta mapato mwaka mzima,” aliongeza.

Katika jukwaa hilo, washiriki walipata pia mafunzo maalum kuhusu sheria, taratibu za manunuzi na mikataba, kupitia warsha iliyoendeshwa na Bw. Paul Bilabaye, Mkufunzi kutoka taasisi ya Uongozi ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya CHAN.

“Sekta hii ya Utalii wa Matukio ina fursa nyingi sana kwa Watanzania. Suala la kuzingatia ni utoaji wa huduma bora katika kila eneo” alisema Paul.
Aliongezea kwa kuwakumbusha wadau kuhusu umuhimu wa kuzingatia utekelezaji wa vifungu vya mikataba wanayoingia katika kazi hizi.

“Ukipata zabuni leo ukaharibu,unakua umeiharibu sifa ya nchi na sio ya kampuni yako pekee,”aliongezea.

Aidha, jopo la majadiliano lililoandaliwa liliwahusisha wataalamu kutoka TTB, BASATA, TRA na BRELA, likiwa na lengo la kurahisisha usajili wa biashara na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.
Jukwaa hilo lilihitimishwa kwa tafrija ya Networking Cocktail Reception, ambapo wadau walipata fursa ya kujenga ushirikiano wa kibiashara kwa siku zijazo.

Tukio hili limeandaliwa na Popular Links kwa kushirikiana na Alliance Française Dar es Salaam na BASATA, na limepongezwa na wadau wengi kama hatua ya kimkakati ya kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya utalii wa mikutano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news