DAR-Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imeokoa wastani wa shilingi bilioni 56.4 kila mwaka ambapo kwa miaka minne ni shilingi bilioni 225.6 zilizokuwa zinapotea kutokana na upotevu wa mafuta bandarini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon Mulokozi ameyasema hayo leo Agosti 7,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wakala, wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema kuwa, kuokolewa kwa fedha hizo kumetokana na kufungwa kwa mifumo ya kisasa ya kutambua kiwango halisi cha mafuta yanayopokelewa kwenye hifadhi za mafuta kutoka melini, hivyo kudhibiti udanyanyifu katika kiasi cha mafuta yanayopokelewa kwenye maghala ya kuhifadhia mafuta nchini.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, kuna ongezeko la kiwango cha uagizaji wa mafuta nchini kupitia Mfumo wa Uagizaji kwa Pamoja (Bulk Procurement System-BPS) kufikia mwaka 2024 kiwango hicho kimefikia tani 6,365,986 kutoka wastani wa tani 5,805,193 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 9.6.
Amesema kuwa, hadi kufikia Desemba 2025, inatarajiwa kuwa kiasi cha tani 7,090,165 kitakuwa kimeagizwa, ongezeko la asilimia 11.4 ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Mulokozi ameeleza kuwa,maboresho yaliyofanyika yameongeza ufanisi wa mfumo huo, na hivyo kuimarisha imani ya mataifa jirani katika kutumia mfumo huo kwa ajili ya uagizaji wa mafuta ghafi.
Kuhusu PBPA
Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA) ulianzishwa mwaka 2015 kwa Amri ya Serikali (Establishment Order,2015) chini ya Mwongozo wa Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agencies Act, (Cap.245) kwa lengo la kuratibu na kusimamia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja.
Sambamba na kuhakikisha ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi ili kupata manufaa ya kiuchumi na upatikanaji wa mafuta nchini wakati wote.
Tags
Habari
Ofisi ya Msajili wa Hazina
PPBPA
Uwekezaji Bandarini
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)
