TANGA-Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, wamemuidhinisha Wallace Karia kuendelea kuwa Rais wa shirikisho hilo kwa miaka mingine minne.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kiomoni Kibamba ametangaza hilo muda mfupi baada ya wajumbe wote wa mkutano huo kumuidhinisha.
“Mkutano mkuu huu leo hii na mahala hapa na muda huu wamemuidhinisha Wallace Karia kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa miaka mingine minne,” amesema Kibamba.
Katika hatua nyingine Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amemteua tena Athumani Nyamlani kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Rais anateua wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji ambao wanathibitishwa na Mkutano Mkuu wa TFF na miongoni mwa wajumbe hao anatoka Makamu wa Kwanza wa Rais.
Nyamlani ametangazwa leo kushika wadhifa huo kwenye Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika jijini Tanga ikiwa ni awamu ya pili, ambapo mara ya kwanza aliteuliwa mwaka 2021.










