ARUSHA-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ametoa wito kwa vijana nchini kushiriki kikamilifu katika masuala ya uwajibikaji wa umma na mapambano dhidi ya rushwa, akisisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu katika kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za taifa.
Akizungumza 14 Agosti 2025 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Uwajibikaji kwa Vijana 2025 linaloandaliwa na Youth Accountability Initiative Forum (YAIF), Prof. Mkenda amesema kuwa rushwa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa, na kwamba vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuikataa na kuikemea.
"Vijana wanapaswa kutambua nafasi yao muhimu katika kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma. Uwajibikaji si jukumu la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania, hususan vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa,"alisema Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda amepongeza YAIF kwa kuratibu jukwaa hilo lenye dhamira ya kuwahamasisha vijana kushiriki katika mijadala ya uwajibikaji, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili, uzalendo, na uelewa wa masuala ya utawala bora.
Prof. Mkenda pia aliwapongeza washiriki wa shindano la uandishi wa insha lililobeba maudhui ya “The Role of Public Accountability in the Proper Management of Public Resources” pamoja na Klabu Bora ya Mwaka 2024/2025 kwa mchango wake katika kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji kwa vijana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIBU, FCPA. Ludovick Utouh, ameeleza kuwa ushiriki wa vijana ni nguzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa uadilifu, uwazi na kwa manufaa ya wote, na kwamba taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wengine kuimarisha misingi ya uwajibikaji nchini.
Jukwaa hilo limehudhuriwa na vijana kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, na limejikita katika kuendeleza mijadala ya uwajibikaji, uwazi, na uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma.
