DAR-Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Minaki na Shule ya Sekondari Dar es Salaam wametembelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, ambapo walipata fursa ya kujifunza kwa undani kuhusu majukumu ya Benki Kuu katika kusimamia uchumi wa nchi na utekelezaji wa Sera ya Fedha.
Katika mafunzo waliyopatiwa, wanafunzi walielimishwa juu ya umuhimu wa kuweka akiba, nidhamu ya kifedha na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani ya sekta ya fedha.
Elimu hiyo imelenga kuwajengea uelewa wa mapema kuhusu masuala ya fedha na mchango wake katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Vilevile, wanafunzi hao walitembelea Makumbusho ya Benki Kuu, ambapo walipata historia ya fedha nchini Tanzania, kuanzia matumizi ya mifumo ya jadi ya biashara ya kubadilishana bidhaa, kuanzishwa kwa sarafu na noti za kwanza, hadi mageuzi makubwa ya kifedha yaliyotekelezwa katika nyakati tofauti.
Pia, walijifunza namna majukumu ya Benki Kuu yamepanuka tangu kuanzishwa kwake, sambamba na mageuzi ya sekta ya fedha nchini.





