Wanufaika wa bima nchini waongezeka kutoka milioni 14 hadi 25.9

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware amesema, wanufaika wa huduma za bima nchini wameongezeka kutoka milioni 14 mwaka 2021 hadi milioni 25.9,mwaka jana huku hamasa ikiendelea ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.
Dkt.Saqware ameyasema hayo leo Agosti 18,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Pia, amesema mali na mitaji katika soko la bima imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.2 mwaka 2021 hadi trilioni 2.3,mwaka huu.

"Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji mzuri wa sera chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mafanikio haya yapo kitakwimu zaidi."

Amesema, pia mafanikio hayo yanatokana na hamasa na elimu inayotolewa na mamlaka kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari nchini.

Vilevile, Dkt.Saqware amesema, idadi ya watoa huduma imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,425 mwaka huu ambapo kuna ongezeko la watoa huduma mpya ikiwemo afya, kidijitali, na bima mtawanyo kutoka moja hadi nne.

Pia, kuna ongezeko la kampuni za bima kutoka 32 mwaka 2021 hadi kampuni 35 huku wawekezaji wengi wakivutiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

Jambo lingine, Dkt.Baghayo Saqware amesema, Serikali imefanikiwa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na kanuni zake.

"Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya 2023 inatoa nafasi kaa wananchi kupata huduma za afya kwa wingi na sahihi, na sheria hii inaenda kuongeza watumiaji wa huduma za afya, kuboresha maisha ya wananchi hasa watakapopata kadi za afya. Aidha, sheria hiyo inatoa nafasi NHIF kuwa chini ya uangalizi wa TIRA."

Aidha, amesema Serikali imefanikiwa kufanya maboresho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022. Serikali iliona ni muhimu kwa miradi yake inayotekelezwa nchini kuwa inakatiwa bima ili kuilinda pamoja na miundombinu.

Dkt.Saqware amesema, jambo lingine ni kuanzishwa kwa consortium ya kilimo ambayo ina kampuni 15 na consortium ya mafuta na gesi ambapo kuna umoja wa kampuni 22 ili kushiriki katika uchumi wa mafuta na gesi nchini kama sekta.

Katika hatua nyingine, amesema wamefanikiwa kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA kutokana na maelekezo ya Rais Dkt.Samia ambapo mamlaka imepiga hatua kubwa na imeweza kuunganisha mfumo wake na Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, LATRA,TASAC na NIDA.

"Matarajio ni kuunganisha taasisi zaidi ya 30 bara na visiwani ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi."

Kupitia kikao kazi hicho, TIRA imebainisha kwa kina mafanikio yake, ilipotoka,ilipo na inapoelekea

"Pili niishukuru sana Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwa dhati kabisa wamekuwa wasimamizi wazuri kwetu."

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), chini ya Sheria ya Bima, Sura ya 394 ina jukumu la kuendeleza sekta ya bima Tanzania Bara na Zanzibar.

Pia, ni taasisi ya Serikali ilioanzishwa ili kutekeleza majukumu ya kusimamia soko na kuendeleza biashara ya bima nchini na masuala yanayohusiana na bima kwa mujibu wa sheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majukumu mengine ni kusajili kampuni za bima nchini, kusimamia na kukagua mwenendo wa kampuni za bima nchini, kutoa elimu ya bima kwa umma, kuhakikisha uendelevu, uhimilivu na usalama wa soko la bima nchini. Vilevile, kuishauri Serikali kuhusu masuala ya bima hapa nchini.

Sabato Kosuri

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Sabato Kosuri amesema kuwa,ustawi wa taasisi za umma unategemea mahusiano mazuri na vyombo vya habari, kwani ni daraja muhimu katika kuunganisha umma.

"Mikutano hii ni chachu ya kuongeza ushirikiano na kuimarisha ushirikiano, hivyo tunaamini mikutano hii ni daraja nzuri la kufikia umma."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news