Waziri Kombo akutana na wabunge marafiki wa Afrika wa Bunge la Japan

YOKOHAMA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wabunge Marafiki wa Umoja wa Afrika katika Bunge la Japan, Mhe. Yamagiwa Daishiro (Mb) tarehe 21 Agosti 2025 pembezoni mwa Mkutano wa TICAD9 jijini Yokohama.
Mheshimiwa Waziri Kombo na Mheshimiwa Yamagiwa pamoja na wabunge wa jumuiya hiyo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Japan katika sekta za teknolojia ili kuleta mabadiliko ya kidijitali; afya; jumuiya za kimataifa kwenye ajenda zenye manufaa kwa pande zote mbili; uendelezaji rasilimali watu; utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo nchini Tanzania kwa mfumo wa ubia wa sekta za umma na binafsi.
Vilevile, walijadili umuhimu wa Japan na Tanzania kushirikiana katika usalama wa chakula hususan kwenye kuongeza uzalishaji, uhifadhi wa mazao na kutafuta masoko ya mazao ya kilimo.

Tanzania itashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo cha Bustani yajulikanayo kama International Horticulture Expo au Green Expo ambayo yatafanyika mwaka 2027 jijini Yokohama.
Maonesho hayo yatatoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya bustani kushirikiana katika teknolojia ya kuzalisha mazao hayo na kupata masoko ya mazao hayo kwa Japan na nchi nyingine duniani ambazo zinaendelea na maandalizi ya ushiriki wa maonesho hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news