NA LWAGA MWAMBANDE
IFAHAMIKE kuwa, Mungu ndiye aliyeumba kila kitu, na ndiye anayetoa maisha na kuongoza maadili ya binadamu.
Ni kwa msingi huo,kumwasi Mungu ni sawa na kuasi mamlaka ya juu kabisa, ambayo ni ya haki,upendo, yenye ujuzi kamili na ni kuvunja agano au amri zake.
Vilevile,kumwasi Mungu ni kinyume kabisa na kumpenda Mungu,pia kutotii ni ishara ya kukataa uongozi Wake, na hiyo ni dhambi.
Rejea katika Biblia Takatifu kitabu cha 1 Samweli 15:23, neno la Mungu linasema,
“Kwa maana uasi ni kama dhambi ya uchawi, na ukaidi ni kama ukosefu wa maana na vinyago...”
Mfano katika Agano la Kale, Mungu aliweka wazi kuwa baraka zinatokana na utii, na laana kutoka kwa uasi.
Rejea katika. Kumbukumbu la Torati 28:1-14 na 28:15-68...“Itakuwa, utakaposikia kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako... atakubariki...”
“Lakini itakuwa, usiposikia sauti ya Bwana, Mungu wako... laana hizi zote zitakujilia...”
Aidha, ifahamike wazi kuwa,kumwasi Mungu ni kukataa makusudi njia ya upendo na hekima aliyoweka kwa ajili ya ustawi wetu, hivyo matokeo ya dhambi ni madhara binafsi na kijamii.
Mathalani,kwa mtazamo wa maadili, kumwasi Mungu mara nyingi huambatana na kuvunja kanuni ambazo zinasaidia jamii kuishi kwa amani kama kusema uongo, kuua, wizi, dhuluma na matendo mengine maovu.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, tukiziungama dhambi zetu, Mungu yeye ni mwaminifu na wa haki hata atusamehe dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote, hivyo kamwe Mungu tusimwasi. Endelea;
1. Tusipitwe nao ng’ombe, tusipitwe nao punda,
Mungu vema atuimbe, jinsi tunavyompenda,
Kuwa na sisi atambe, tuzae mema matunda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
2. Vipi amsifu ng’ombe, bwana wake kumpenda,
Huyu dhalili kiumbe, ajue jinsi ya kwenda,
Bali sisi atuchambe, kwake tunavyovurunda?
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwache.
3. Kwamba punda amuimbe, ana bwana ampenda,
Hata lile lake tembe, ajijue akienda,
Halafu sisi tuvimbe, Muumba kutompenda?
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
4. Katika vyote viumbe, duniani kuvipanda,
Havifiki hata chembe, jinsi alivyotuunda,
Katika vyote viumbe, hadhi yetu imepanda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
5. Kwa ustadi atuumbe, viumbe vyote kushinda,
Kisha amtaje ng’ombe, hata kumsifu punda,
Rehema kwake tuombe, ya kwamba tumevurunda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
6. Ni mabingwa tuna kombe, jadhi kwake imepanda,
Vitu vyote hata ng’ombe, twatiisha vinakwenda,
Kwa kiburi tusivimbe, umilele uwe tenda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
7. Kwa Mungu tuwe majembe, kwa moyo tukimpenda,
Tushughulike atambe, kazi tusijevurunda,
Wote walio wazembe, watubu na kumpenda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
8. Sifa za Mungu tuimbe, tuseme anatupenda,
Kama kura za wajumbe, juu azidi kupanda,
Hebu tuache usambe, dunia itatushinda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
9. Tuna akili si ng’ombe, kichwani asijepanda,
Kwa ufahamu tutambe, wala sisi siyo punda,
Tutambue kwamba kumbe, Mungu wetu atupenda,
Atulisha atulea, kamwe Mungu tusimwasi.
(Isaya 1:2-3, Yoeli 2:12, Zekaria 1:3, Malaki 3:7)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
