ZANZIBAR-Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe.Tabia Maulid Mwita amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa kuunga mkono miradi ya maendeleo ya michezo ili ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Mhe. Tabia ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kukagua maeneo yanayotarajiwa kujengwa viwanja vya mpira wa miguu katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema, Serikali inawekeza fedha nyingi katika kuendeleza miundombinu ya michezo kwa manufaa ya wananchi, hivyo ni vyema jamii kutoa ushirikiano ikiwemo kupisha maeneo yanapohitajika kwa ujenzi huo.
Aidha, Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa maslahi ya wanamichezo na Taifa kwa ujumla, huku akiwataka Masheha na Wakuu wa Wilaya zinazohusika kutoa elimu kwa wananchi ili kufanikisha ujenzi huo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Ndg. Ameir Mohammed Makame, amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua maeneo hayo na kubaini changamoto zilizopo ili kupatiwa ufumbuzi.
Ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali pindi utekelezaji wa miradi utakapoanza ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Mhe. Tabia amefanya ziara katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kijini Matemwe, Pwani Mchangani, Kama na Mtoni, ambako Serikali inapanga kujenga viwanja vya wilaya pamoja na uwanja wa mpira wa ufukweni.
