Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kulinda haki za wanawake-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kulinda haki za wanawake kwa kuwa na sera na sheria bora zinazohakikisha usalama, usawa wa kijinsia na kuwepo kwa miji na maeneo salama ya kijamii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 26,2025 wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Dunia wa Miji na Maeneo Salama ya Kijamii na Usalama kwa Wanawake unaofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni ishara ya Jumuiya ya Kimataifa kutambua juhudi za Zanzibar katika kuwalinda wanawake na wasichana kupitia utekelezaji mzuri wa sera na sheria zinazowahakikishia fursa na ustawi wao.
Amefahamisha kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele suala la usawa wa kijinsia kwa kuandaa miji na maeneo salama ya kijamii yanayotoa fursa kwa wanawake kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu, unyanyasaji wa kijinsia na kwa kushirikishwa katika nyanja mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi, wadau na washirika wa maendeleo kuwa Zanzibar ni nchi salama na wananchi wake wanaendelea kutekeleza shughuli za kimaisha kwa amani na utulivu.

Aidha, ameeleza kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na taasisi zenye dhamana ya kuwalinda wanawake na wasichana nchini.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar imeamua kuwawezesha wanawake kwa kuwaandalia mazingira salama katika maeneo wanayofanyia shughuli zao wakati wote.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Taasisi ya UN Women kwa mikakati na juhudi zake katika kuhakikisha wanawake duniani kote wanalindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa wadau, taasisi za kikanda na za kimataifa kuungana kwa lengo la kuendeleza miji na maeneo salama na rafiki kwa maendeleo ya wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news