BERLIN-Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassani Mwamweta amewataka wanariadha wanaoshiriki mashindano ya BMW Berlin-Marathon mwaka 2025 kutetea heshima ya nchi kwa kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri katika mashindano hayo, yatakayofanyika Berlin Septemba 21, 2025.

Balozi Mwamweta kauli hiyo ameitoa alipokutana na wanariadha hao, wakiongozwa na Bw. Gabriel Geay ofisini kwake jijini Berlin leo Septemba 19, 2025.
Balozi Mwamweta amesema, mashindano ya BMW Berlin-Marathon ni miongoni mwa mashindano makubwa ya riadha Duniani ambayo mwaka huu yatajumuisha washiriki 80,000 kutoka duniani kote, hivyo ushindi wa aina yotote utailetea heshima na kuitangaza nchi ya Tanzania ulimwenguni.
Balozi Mwamweta amewatakia heri wakimbiaji hao katika mashindano hayo na kuwaahidi kuwapa ushirikiano unaohitajika ili waweze kuwakilisha vyema bendera ya Taifa. #BerlinMarathon
