BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza Dhamana za Serikali za muda mrefu (Hati fungani) ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa ama taasisi au mwananchi mmoja mmoja.

Dhamana za muda mrefu ni zile ambazo muda wake wa kuiva unazidi mwaka mmoja. Dhamana hizi huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani kupitia minada na baada ya hapo uuzaji wa dhamana hizo hufanywa kwenye soko la upili.
Mwekezaji atanunua Hati fungani kupitia kwa mawakala ambao ni benki zote za biashara zilizosajiliwa na kupatiwa leseni ya biashara na benki kutoka Benki Kuu ya Tanzania au mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam waliopatiwa leseni na kusimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Mwekezaji mwenye kiwango cha kuanzia shillingi milioni moja (TZS 1,000,000.00) na kuendelea anaruhusiwa kushiriki katika mnada wa Dhamana za Muda Mrefu (Hati Fungani).
Kabla ya kuwekeza, kila mwekezaji anatakiwa kufungua akaunti maalum ya uwekezaji inayoitwa Central Depository System Account (Akaunti ya CDS).
