SINGIDA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa elimu kwa watu wenye ulemavu wa kusikia kuhusu majukumu yake ya msingi, katika maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Viziwi Duniani yanayofanyika kitaifa mkoani Singida kuanzia tarehe 22 hadi 27 Septemba, 2025.
Mchumi kutoka Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bi. Regina Mwaipopo, aliwasilisha mafunzo hayo kwa washiriki, ambapo alieleza majukumu ya msingi ya Benki Kuu pamoja na fursa mbalimbali ambazo taasisi hiyo imekasimiwa ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Ushiriki wa Benki Kuu katika kongamano hili ni sehemu ya mikakati endelevu ya BoT ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nafasi yake katika kulinda thamani ya shilingi, kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha, na kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi nchini.

