GEITA-Wataalamu wa Benki Kuu ya Tanzania wameendelea kutoa elimu kwa wananchi mbalimbali wanaotembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Katika banda hilo, wananchi wamepata fursa ya kufahamu majukumu makuu ya Benki Kuu yakiwemo kusimamia sera ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei, kusimamia sekta ya benki na taasisi za kifedha pamoja na kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.
Aidha, wananchi wamepata elimu ya kutambua alama za usalama zilizopo kwenye noti halali za shilingi, jambo linalosaidia kupunguza hatari ya kupokea fedha bandia.
Vilevile, elimu imetolewa kuhusu mpango wa ununuzi wa dhahabu unaoratibiwa na Benki Kuu kwa lengo la kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya shilingi yetu.






