BoT yatoa elimu kwa viongozi wa SMZ kuhusu matumizi ya fedha za kigeni na uwekezaji wa dhamana za Serikali

ZANZIBAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo maalum kwa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) yakilenga ufafanuzi wa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025 pamoja na fursa zilizopo katika uwekezaji wa dhamana za Serikali.
Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 20 Septemba 2025 katika ofisi za BoT Zanzibar, yakiongozwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Mhandisi Zena Ahmed Said.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Bw. Emmanuel Akaro, alieleza kuwa Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za mwaka 2025 zimetolewa chini ya Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.
Alisisitiza kuwa bei na malipo ya bidhaa na huduma zote kwa wakaazi ndani ya Tanzania lazima yafanyike kwa Shilingi ya Tanzania.

Alionya kuwa hairuhusiwi kunukuu wala kulipia kwa fedha za kigeni, na pia ni kosa kukataa Shilingi ya Tanzania kama malipo halali.
Hata hivyo, Bw. Akaro alifafanua kuwa malipo kati ya wakaazi na wageni, ikiwemo watalii, yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

Aidha, mawakala wa utalii waliopo nchini wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni kulipia huduma kwa niaba ya wateja wao kutoka nje ya nchi.
Kuhusu uwekezaji katika dhamana za Serikali, Bw. Akaro alieleza kuwa, ni njia salama na yenye uhakika kwa wawekezaji, kwa kuwa Serikali haitarajiwi kukiuka makubaliano ya malipo.

Aliongeza kuwa, dhamana hizo zinahamishika, hivyo mwekezaji anaweza kuziuza kabla ya muda wake wa kuiva endapo ataona inafaa.

Pia, alibainisha kuwa dhamana za Serikali zinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo kupitia taasisi mbalimbali za fedha, huku zikiwa na kiwango cha faida kinachovutia kwa wawekezaji.
Mafunzo haya yamelenga kuongeza uelewa wa viongozi wa SMZ kuhusu matumizi sahihi ya fedha za kigeni na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika fursa za uwekezaji zinazotolewa na Serikali kupitia BoT.

Semina hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Benki Kuu ya Tanzania, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Tawi la Benki Kuu Zanzibar, Bw. Ibrahim Malogoi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news