DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki Kuu ya Malawi (RBM) ulioongozwa na Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa RBM, Bi. Chakudza Linje, walipotembelea ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam tarehe 2 Septemba 2025.
Lengo la ziara ya ujumbe huo ni kujifunza namna BoT inavyotekeleza mpango wa ununuzi wa dhahabu, na jinsi Malawi inaweza kutumia uzoefu huo ili kuanzisha mpango kama huo nchini kwao.Mpango huu umeleta mafanikio makubwa katika kuongeza hifadhi ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya Shilingi ya Tanzania. Kufuatia kuanza kwa utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Madini, Kifungu cha 59, mnamo tarehe 1 Oktoba 2024, Benki Kuu ilianza rasmi ununuzi wa dhahabu kupitia mpango huu.
Hadi kufikia Agosti 2025, jumla ya tani 9.165 za dhahabu zenye thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 1,015.98 zimekwishanunuliwa.



