BoT yazidi kupaisha uchumi kwa teknolojia bunifu za malipo

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kurekodi mafanikio makubwa kupitia bunifu katika teknolojia za malipo ambazo zimechochea ongezeko kubwa la miamala nchini kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Takwimu zinaonesha kuwa, jumla ya miamala milioni 560 yenye thamani ya shilingi trilioni 41 ilifanyika katika kipindi hicho.
Hayo yamesemwa leo Septemba 16,2025 na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Kuu, Bi.Lucy Shaidi wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo bunifu za mifumo ya kisasa ya malipo zimeiwezesha BoT kutunukiwa Tuzo Kuu ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha (Nestor Espenilla Jr. Financial Inclusion Innovation Award).

Tuzo hiyo ilipokelewa na Naibu Gavana anayesimamia Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Huduma Jumuishi za Fedha uliofanyika mjini Swakopmund, nchini Namibia mwanzo mwa mwezi Septemba,2025.

Vilevile, Bi.Shaidi amesema, miamala kupitia huduma za msimbomilia na LipaNamba imefikia milioni 60 yenye thamani ya shilingi trilioni 4.

Hatua hizo zimewezesha maboresha ya huduma za kifedha kwa kuongeza usalama na urahisi wa malipo kwa watumiaji kote nchini.

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kukuza uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi, na hivyo kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine za kuchangia matumizi ya huduma jumuishi za fedha, amesema Benki Kuu imeanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu (Bank of Tanzania Fintech Regulatory Sandbox Regulations, 2024) ili kuchochea wabunifu kuweza kujaribu bunifu zao.

Kadhalika Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa huduma bora imeanzisha mfumo maalumu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi (SEMA na BoT) ili kuhakikisha kero za wananchi juu ya huduma za fedha zinashughulikiwa kwa wakati.

Amebainisha kuwa, mafanikio haya ni kielelezo cha uongozi thabiti wa Benki Kuu chini ya Gavana Emmanuel Tutuba katika kusimamia juhudi za kuongeza na kuchochea matumizi ya huduma za fedha kwa kutumia teknolojia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news