GEITA-Mkuu wa Wilaya ya Geita (DC), Mhe. Hashim Komba ametoa wito kwa taasisi za usimamizi wa sekta ya fedha kuhakikisha zinasimamia hadi kwenye taasisi ndogo za wananchi (VICOBA) ili kuepuka hasara ambazo zinatokea kutokana na kukosa usimamizi madhubuti.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, akisikiliza maelezo kutoka Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Bw. Lwaga Mwambande, wakati alipotembelea banda la DIB katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mjini Geita leo Septemba 26, 2025.
Mheshimiwa Komba ameyasema hayo leo Septemba 26,2025 alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mjini Geita.
“Tumekuwa tukipata malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamejiwekea hisa zao katika Vicoba, pengine mmojawapo anatoroka na fedha na inakuwa kazi kumtafuta,”amesema Bw.Komba na kutaka taasisi za udhibiti kuhakikisha kwamba wanafika hadi huko ili kuleta utulivu.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, akipokea zawadi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw.Lwaga Mwambande alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita tarehe 26 Septemba 2025. Wengine katika picha ni Maafisa wa DIB, Bi. Kulwa Kasuka na Bi. Shamimu Makongoro.
Ameitaka DIB kushirikiana na BoT na taasisi nyingine za usimamizi kuhakikisha kwamba usimamizi madhubuti unafika hadi kwenye ngazi za Vicoba ili kuondoa sintofahamu zinazojitokeza katika vikundi hivyo.
Bw. Komba ameipongeza, Bodi ya Bima ya Amana kwa kazi zake ambazo alisema zinaongeza imani ya wananchi katika kutumia huduma za kifedha zinazotolewa na benki na taasisi za fedha.
Amesema kuwa, ana uhakika kwamba mtu akiwa na akaunti yake benki, halafu benki ikafungwa au kufilisika anaweza kupata fedha zake ni jambo jema sana.
Mapema Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Bw. Lwaga Mwambande amemweleza Mkuu huyo wa Wilaya kwamba, Bodi ya Bima ya Amana inakinga amana za wananchi katika benki na taasisi za fedha dhidi ya hasara ambayo inaweza kutokea endapo taasisi kama hizo zitafungwa au kufilisika.
Tofauti na bima nyingine, wachangiaji katika Mfuko wa Bima ya Amana ambao unasimamia na DIB ni benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakati wateja wa benki na taasisi za fedha hizo ni wanufaika tu wa fidia endapo benki ikifilisika.
Majukumu mengine ya Bodi ya Bima ya Amana ni kuendesha zoezi la ufilisi wa benki au taasisi ya fedha endapo ikiteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja kupunguza hasara kwa benki au taasisi ya fedha ambayo inapitia changamoto zinazotishia usalama wake.
Kwa mujibu wa uzoefu, jukumu la kuhusika na kupunguza hasara (Loss Minimiser) linasaidia siyo tu kunusuru benki zisife au kufilisika, bali pia linaweza kuwa la gharama nafuu kuliko zoezi la fidia na ufilisi baada ya benki kushindwa kufanya kazi, mtawali.
Tags
Bodi ya Bima ya Amana (DIB)
Deposit Insurance Board
(DIB)
Habari
Maonesho ya Madini Geita
The Deposit Insurance Board (DIB)



