GEITA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Mara baada ya kuwasili, Dkt. Biteko alipokelewa na Meneja wa Idara ya Mawasiliano wa Benki Kuu, Bi. Victoria Msina, ambaye alimueleza kwa kina kuhusu huduma na elimu zinazotolewa kwa wananchi wanaotembelea banda hilo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko alipata fursa ya kujionea namna wataalamu wa BoT wanavyotoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya Benki Kuu, ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei, kusimamia sekta ya fedha, na kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.
Benki Kuu imeendelea kushiriki katika maonesho mbalimbali nchini kwa lengo la kuendeleza mawasiliano na jamii, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sekta ya fedha na nafasi yake katika kukuza uchumi wa taifa.

