Rais Dkt.Samia ni mama wa maendeleo, Dkt.Mwinyi ni daktari wa maendeleo-Majaliwa

ZANZIBAR-Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha kuwa ni mama wa maendeleo kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi nchini.
Ameyasema hayo Septemba 27,2025 wakati akihutubia wananchi Jimbo la Kojani kisiwani Pemba.

Majaliwa amesema,Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha ujenzi wa vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma zote za msingi, hali iliyopunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

“Kwa sasa wananchi hawaendi umbali mrefu kupata huduma za afya, wataalamu wa afya wameajiriwa,”alisema.

Alibainisha kuwa, Rais Dkt. Samia ametekeleza pia maono yake ya kumtua mama ndoo kichwani kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa, ya kati na midogo ya maji, sambamba na kuvutia wawekezaji waliowekeza katika miradi mikubwa iliyotoa ajira kwa Watanzania.
Majaliwa alisisitiza kuwa, Rais Dkt.Samia ni mgombea pekee mwenye maono ya kuivusha Tanzania, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 29,2025.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimpongeza mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar,Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuifungua Zanzibar kiuchumi na kugusa sekta mbalimbali za kijamii.

“Uongozi wa Dkt. Mwinyi umegusa kila sekta ikiwemo miundombinu, elimu, afya, maji, michezo na huduma nyingine. Ni Daktari wa Maendeleo, nendeni mkamjazie kura,” alisema.

Aidha, Majaliwa alimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kojani, Hamad Chande, akimtaja kuwa ni mtendaji, mzalendo na mchapa kazi.
“Ninamfahamu Chande. Ndiyo maana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Mchagueni ili aendelee kuwaletea maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake, Chande aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuendelea kuwa mbunge wao, akiahidi kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news