ZANZIBAR-Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi leo Septemba 30,2025 amekutana na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Soko la Kibanda Maiti lililopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dkt.Mwinyi amewaahidi maboresho makubwa katika sekta ya biashara ndogo na za kati katika awamu ijayo ya uongozi wake.
Dkt.Mwinyi amewaahidi maboresho makubwa katika sekta ya biashara ndogo na za kati katika awamu ijayo ya uongozi wake.Katika hotuba yake kwa wananchi waliokusanyika sokoni hapo, Dkt.Mwinyi amesema kuwa,tayari Serikali imekamilisha michoro ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Kibanda Maiti na kwamba fedha za kutosha zimetengwa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango bora.
“Serikali imejipanga kufanya kazi ya ziada katika awamu ijayo ili kuwawezesha zaidi wafanyabiashara na wajasiriamali wetu. Hatua hizi ni pamoja na ujenzi wa masoko ya kisasa na upatikanaji wa mikopo isiyo na riba,”amesema Dkt.Mwinyi.
Pia,ameongeza kuwa,Serikali itaimarisha zaidi mfumo wa utoaji wa mikopo hasa kwa wafanyabiashara wenye historia nzuri ya urejeshaji, kwa kuwapa fursa zaidi ya kukuza mitaji yao na kupanua biashara.
Dkt. Mwinyi amewataka wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumpa yeye pamoja na wagombea wote wa chama hicho ridhaa ya kuongoza tena ili kuhakikisha utekelezaji wa ahadi hizo unafanyika kwa mafanikio makubwa.
“Nawaomba wananchi kuendelea kuamini Chama Cha Mapinduzi na kunipa tena ridhaa pamoja na wagombea wote wa CCM ili tuweze kutekeleza kwa vitendo ahadi hizi kwa mafanikio makubwa,”amesisitiza Dkt.Mwinyi.
















