ZANZIBAR-Leo Septemba 30,2025 mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekutana na wavuvi,wachuuzi wa samaki na wajasiriamali katika maeneo ya Diko na Soko la Samaki la Malindi.
Katika mkutano huo, Dkt.Mwinyi ameahidi kuendeleza juhudi za kuwawezesha wananchi ili kuongeza kipato chao na kuchangia katika kukuza uchumi wa Zanzibar.Vilevile,amebainisha kuwa serikali itaandaa utaratibu mzuri wa usimamizi wa masoko ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wajasiriamali.
Aidha, Dkt.Mwinyi ametangaza kuwa fedha za mikopo kwa ajili ya wajasiriamali zitaongezwa maradufu kutoka shilingi bilioni 96 zilizotolewa awali, kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila anayeihitaji anapata nafasi, hasa wale ambao hawakunufaika katika awamu ya kwanza.
Katika juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi, Dkt.Mwinyi amesema, serikali itaendelea kujenga madiko na masoko ya samaki katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia, serikali itawekeza katika vifaa vya kisasa, vikiwemo boti na vitendea kazi vya kisasa, ili kuwawezesha wavuvi kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu.

.jpg)












