NA DIRAMAKINI
MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Nabii Dkt. Alphonce Boniface Temba ametangaza rasmi kufuta laana zote zilizowahi kutamkwa na baadhi ya manabii dhidi ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akimtabiria ushindi wa kishindo Oktoba 29,2025.
Amesisitiza kuwa,Watanzania wanapaswa kufahamu na kuwatofautisha manabii,kwani kuna aina tofauti za manabii ambao wasipokuwa makini watajikuta wakipotoshwa.
"Ukisoma Biblia kitabu cha Mathayo 16:23 neno la Mungu linasema...Akageuka, akamwambia Petro,nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu."
Aidha, amesema Nabii huwa analeta jambo ambalo halikuwepo kabla na si mtu kuibuka katikati ya tukio mfano uchaguzi wakati kampeni zikiendelea na kutoa unabii.
Dkt.Temba ni kati ya manabii ambao Mungu amekuwa akiwapa jumbe mbalimbali za uchaguzi barani Afrika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mfano aliwahi kutabiri huko Malawi, Zambia, DR Congo, Kenya, Botswana,Tanzania.
Akizungumza Septemba 14,2025 katika kampeni za kuwaombea kura mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan,ubunge Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Angellah Kairuki.

Sambamba na madiwani wa chama hicho katika Kata ya Kwembe, Dkt.Temba amewataka manabii kuacha kutumia vibaya neno la Mungu kwa faida zao binafsi, akisisitiza kuwa uongozi wa Dkt.Samia ni baraka kwa taifa.
“Rais Samia amekirimiwa kipawa cha uongozi kutoka kwa Mungu. Hii ndiyo sababu taifa letu limeendelea kuwa na umoja, amani, mshikamano na usalama,"amesema Dkt.Temba huku akihimiza Watanzania kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo huku akitolea mfano namna Simba Day na Mwananchi Day zilivyofanyika usiku wa manane na wananchi wakarejea majumbani kwa amani kitu ambacho ni nadra kwa mataifa mengi ya Afrika.
Nabii huyo pia amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili na kueneza ujumbe wa upendo, badala ya kutumika kwa ajili ya ajenda binafsi zinazowagawa wananchi.
Kauli hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi, huku wengi wakieleza kuwa ni wakati muafaka kwa jamii kuungana na kuombea viongozi badala ya kuwahukumu bila sababu za msingi.
Pia, Dkt.Temba amesisitiza kuwa ni wakati sasa wa viongozi wa dini kuhubiri amani na si chuki.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kumuombea na kumuunga mkono Dkt.Samia ili aendelee kuliongoza taifa kwa mafanikio makubwa zaidi.
Dkt.Temba amesema,Rais Samia amepewa neema ya kipekee ya uongozi, na kwamba taifa linaendelea kufurahia matunda ya amani, mshikamano na usalama chini ya uongozi wake.
"Endapo Mungu anataka kumlaani Mfalme au kiongozi mkubwa kwa maana ya Rais baada ya kuwa amefanya kosa, Mungu huwa anatuma onyo kwake kwa maana atubu au aache kile ambacho kinamfanya Mugu ampe hiyo adhabu."
Amesema,Mungu anapotuma hilo onyo, anapolipokea au akalidharau na kulipinga ndipo Mungu baadaye huwa analeta hasira yake.
"Lakini,haiwezekani Mungu tu kuleta hasira juu ya kiongozi ambaye amempa baraka pia ya kuongoza na baraka ya kuaminiwa na watu na hata kupigiwa kura, halafu Mungu akajichanganya tena huko akamlaani, hicho kitu hakiwezekani.
"Ni kwamba kama kuna Mfalme amemkosea Mungu, Mungu anapeleka maonyo kwake na anaona moyo wake kwamba huyo mtu amepokea toba au amebadilika au la sivyo, Mungu anafanya kuishusha hasira yake.
"Lakini siyo watu kuibuka tu kwenye mitandao na hakuna meseji za kwenda kimitandao, zaidi ya kwenda personal au kutumwa taarifa kwa muhusika kama kulikuwa na kosa lolote, hilo kosa lingeenda kwa muhusika moja kwa moja kutoka kwa Mungu, au kutumwa taarifa kwa muhusika kama kulikuwa na kosa lolote na endapo anapinga, ndipo hapo Mungu angetumia hasira yake kwa adhabu yoyote.

"Kwa hiyo, vinavyotendeka kwenye mitandao ninataka Watanzania wajue huo si utaratibu wa ki Mungu na ninafuta hizo laana zote zinazosemwa vibaya na kuwatia Watanzania hususani Wakristo hofu na kuwafanya wachanganyikiwe kwamba hilo ni suala ambalo linaingia kimkakati sana, kwa maana ya hizo laana zinazosemwa zimekuwa na uwalakini, kwa hiyo tunaamini kabisa Mungu atambariki kiongozi wetu na hatakufa na atakakuwa kiongozi na atastaafu kwa heshima," amesisitiza Dkt.Temba.
Katika hatua nyingine Nabii Dkt.Temba amemuombea kura Dkt.Samia, Mheshimiwa Angellah Kairuki, madiwani wote wa Kibamba huku akisisitiza kuwa,viongozi hao ambao waneaminiwa na chama wana uwezo mkubwa wa kushirikiana nao kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.
Hata hivyo, Dkt.Temba ambaye ni kati ya watia nia Jimbo la Kibamba ambao kura zake hazikutosha amekabidhi bendera 300 za chama kwa Katibu wa chama Wilaya ya Ubungo ili kusambazwa katika kata sita Jimbo la Kibamba huku akichangia zaidi ya shilingi milioni 1 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za chama kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
.jpg)

